Mkuu wa Sera za Nje wa EU: Israel imekiuka sheria za kimataifa katika shambulio la Beirut lililoua watu 7
Oct 04, 2024 09:39 UTC
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya (EU) Josep Borrell amelaani shambulizi lililofanywa na Israel katika mji mkuu wa Lebanon Beirut lililoua watu saba na kulielezea kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X, Borrell amesema: "kwa usiku mmoja, IDF ililenga tena wafanyakazi wa sekta ya afya katikati mwa Beirut: watu 7 wakiwemo wahudumu wa afya waliuawa".
Huku akisisitiza kuwa analaani ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ameongezea kwa kusema: "raia sio tu ndio waathirika wa mashambulizi, ikiwa ni pamoja na yanayolenga maeneo yenye watu wengi, lakini pia wanakoseshwa huduma za dharura".
Wahudumu saba wa sekta ya tiba wa kituo cha Mamlaka ya Afya ya Kiislamu chenye mfungamano na harakati ya Hizbullah waliuawa shahidi katika shambulizi la jeshi la Israel dhidi ya kituo cha ulinzi wa raia katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut jana Alkhamisi.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha mashambulizi makubwa ya anga tangu Septemba 23 dhidi ya kile unachokiita kuzilenga ngome za Hizbullah katika kila pembe ya Lebanon, na kuua zaidi ya watu 1,100 na kuwafanya maelfu ya wengine walazimike kuyahama makazi yao.
Siku ya Jumanne, vikosi vya jeshi vamizi la utawala wa Kizayuni wa Israel vilianza kuivamia Lebanon kupitia ardhini, hatua ambayo imepelekea makumi ya wanajeshi wa utawala huo haramu kuangamizwa katika mapigano na wanamuqawama wa Hizbullah.../