Venezuela yahimiza kuundwa 'harakati ya dunia' kukabiliana na ugaidi, unyama wa Israel
Serikali ya Venezuela imesisitiza ulazima wa kuungana mkono baina ya Iran na mataifa ya Kiarabu Asia Magharibi ili kuanzisha "harakati ya dunia" dhidi ya uhalifu na vitendo vya ugaidi vya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Yvan Gil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ametoa wito huo baada ya kukutana na mabalozi na wawakilishi wa kidiplomasia wa Iran, Palestina, Lebanon, Syria, Kuwait, Algeria, Misri, Saudi Arabia, Iraq, Qatar na Sudan katika mji mkuu, Caracas siku ya Ijumaa.
Akizungumza katika mkutano huo, ambao ulifanyika kwa ombi la Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, Gil alitaja kuundwa kwa "harakati kubwa ya dunia ambayo inalaani mauaji" na kutumia rasilimali zote zilizopo katika diplomasia "kuuzuia utawala ambao utasimamishwa tu kwa uhamasishaji wa kimataifa.”
Ameendelea kusema kuwa: "Kikosi hiki lazima kiwe nguvu ya kidiplomasia ili kukomesha unyama huo. Katika siku zijazo, hatua madhubuti zitachukuliwa kuzuia 'utawala wa Kinazi' wa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu".
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Venezuela amesema: "Mwaka mmoja uliopita, utawala wa kifashisti (wa Israel) ulianza awamu ya awali ya kuwaangamiza Waislamu wote ambapo mbinu mbaya zaidi za vita zimetumika, ikiwa ni pamoja na matumizi ya ndege zinye mabomu makubwa kuangamiza wakazi wa mji mzima."

Gil amesisitiza kwamba kinachofanyika katika Ukanda wa Gaza kinafanyika pia nchini Lebanon, na "mauaji haya ya kimbari yameendelezwa kwa msaada wa Marekani, kwa ukimya wa Umoja wa Ulaya na jamii ya kimataifa."
Amesema: "Ubinadamu hauwezi kuvumilia kifo kimoja zaidi na bomu moja zaidi kuanguka kwenye vichwa vya wasichana na wanawake wa Kipalestina."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ameutaja uchokozi wa Israel dhidi ya Gaza na Lebanon kuwa ni shambulio kubwa zaidi dhidi ya ubinadamu tangu baada ya kiongozi wa Unazi, Adolf Hitler, na kuongeza kuwa: "Inaonekana kwamba tuna Hitler mpya anayeungwa mkono na madola ya Magharibi."
Mwanadiplomasia huyo wa Venezuela pia ametumia akaunti yake ya Telegram na kusema Caracas itaendelea kuunga mkono hatua dhidi ya Israel na Marekani katika eneo la Asia Magharibi.