Katibu Mkuu wa UN: Sasa ni wakati wa kunyamazishwa sauti za bunduki Mashariki ya Kati
Katika mkesha wa kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa mashambulizi ya Oktoba 7, 2023, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kukomesha mara moja "umwagaji damu na ukatili wa kutisha" katika ukanda wa Gaza na Lebanon, kunyamazisha sauti za bunduki na kurejeshwa amani katika eneo hilo.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema katika taarifa yake ya leo Jumapili kwamba vita vilivyoanza mwaka mmoja uliopita vinaendelea kuharibu maisha ya watu na kusababisha mateso makubwa kwa Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza, na sasa kwa watu wa Lebanon.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, baada ya Oktoba 7 kulitokea wimbi la kustaajabisha la umwagaji damu na ukatili, na kuongeza kuwa, sasa ni wakati wa kuachiliwa huru mateka; Ni wakati wa kunyamazisha bunduki na kukomesha mateso yaliyolikumba eneo hilo, na ni wakati wa amani, utekelezaji wa sheria na haki za kimataifa.
Itakumbukwa kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianza vita vikali dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, na katika mwaka mmoja uliopita, asilimia 70 ya nyumba na miundombinu ya eneo hilo imeharibiwa vibaya katika vita hivo, huku mzingiro mkubwa na mgogoro mkubwa wa binadamu pamoja na njaa isiyo na kifani vikiendelea kutishia maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Licha ya jinai zote hizo, Israel imekiri kwamba baada ya takriban miezi 12 ya vita bado haijaweza kufikia malengo yake ya vita hivyo ambayo ni kuiangamiza harakati ya Hamas na kuwarejesha mateka wa Kizayuni kutoka Ukanda wa Gaza.
Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza Jumamosi kwamba tangu tarehe 7 Oktoba 2023, Israel imeua shahidi Wapalestina wasiopungua 41,825 na kujeruhi wengine zaidi 96,910.