Ulazima wa kuwekewa vikwazo na kufukuzwa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa
Wigo wa jinai za kivita za utawala wa Kizayuni huko Gaza na kupanuka jinai hizo hadi Lebanon, jambo ambalo linakinzana waziwazi na misingi ya Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, hauhalalishi kwa namna yoyote kuendelea kuwepo utawala huo katika Umoja wa Mataifa na katika taasisi nyingine za kimataifa.
Katika hali ambayo vita dhidi ya Gaza vimeingia katika siku yake ya 374; jeshi la utawala ghasibu wa Israel linaendelea kushadidisha oparesheni zake za kijeshi kaskazini mwa ukanda huo.
Kwa siku 9 sasa utawala ghasibu wa Israel umezingira maeneo ya Jabalia, Bait Hanoun na Bait Lahia kwa kutekeleza mpango kwa jina la " Mkakati wa Majenerali" ili kuandaa zoezi la kuwahamisha kwa nguvu katika makazi yao na kuwafanya wakimbizi Wapalestina na kuanza kutenganisha eneo la kaskazini mwa Gaza na ukanda huo mzima.
Katika upande mwingine, licha ya wanajeshi wake kuuawa na kujeruhiwa, utawala huo bado unajaribu kuikalia kwa mabavu ardhi ya kusini mwa Lebanon; na ili kubatilisha Azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama, umewashambulia askari jeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa (UNFIL) ili kuwafurusha katika eneo hilo.
Katika kukabiliana na mashambulio na hujuma hizo, harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imesambaratisha vikosi vamizi; na baadhi ya duru za Israel zimeeleza kuwa askari wa Kizayuni waliojeruhiwa jana asubuhi pekee hawapungui 11 na kwamba walihamishiwa haraka katika hospitali za Haifa.
Nayo tovuti ya World Cargo News imeripoti kuwa: "Bandari ya Eilat ya Israel imetangaza kufilisika kutokana na kupungua shughuli zake kwa asilimia 85 kutokana na mashambulizi ya harakati ya Ansarullah ya Yemen dhidi ya meli katika bahari Nyekundu." Kabla ya hapo viongozi wa Kizayuni walikiri kwamba vita vya Gaza ni vita vilivyowagharimu pakubwa kwa takribani dola bilioni 70 tangu kuasisiwa utawala huo.
Licha ya gharama na hasara zote hizo, utawala wa Kizayuni hauna nia ya kupunguza mashambulizi na mauaji yake ya kimbari na kufikia usitishaji vita ambao kwa kiasi fulani unahusiana na juhudi za kusimamisha vita hadi kufanyika uchaguzi nchini Marekani, na katika upande mwingine unahusiana na uungaji mkono wa pande zote wa serikali ya Biden kwa utawala huo.
Hii ni pamoja na kuwa baadhi ya serikali zilizopita za Marekani zilionyesha angalau kupinga hatua za kujitanua na mabavu za utawala wa Kizayuni kutokana na mashinikizo ya waliowengi ulimwenguni. Eisenhower alipoiwekea Israel vikwazo vya kiuchumi na kijeshi mwaka 1956; Jimmy Carter aliitaja Israel kuwa ni utawala wa kibaguzi, na mwaka 1982 wakati Israel ilipotekeleza mashambulizi dhidi ya Lebanon na kuua Wapalestina na Walebanoni 18,000, Reagan aliyaita mauaji hayo kuwa Holocaust na kuitishia Israel; na utawala huo ukalazimika kusimamisha vita. Kwa msingi huo, John Mersheimer Profesa mtajika katika Chuo Kikuu cha Chicago ameeleza katika uchambuzi wake wa karibuni kuwa lobi ya Wazayuni inaidhibiti kikamilifu Marekani nzima kwa kadiri kwamba hakuna kiongozi yoyote mwenye uthubutu wa kuupinga utawala huo.
Kwa kuzingatia hayo, Marekani ambayo ni muungaji mkono mkuu wa kisiasa na nchi inayoupatia silaha na zana za kijeshi utawala wa Kizayuni, zinazotumika katika mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza na Lebanon ni mshirika wa utawala huo katika kutekeleza jinai kubwa zaidi duniani. Katika mazingira haya, matakwa yaliyowasilishwa na nchi mbali mbali kwa ajili ya kuuwekea vikwazo vya silaha utawala wa Kizayuni pia yanapaswa kuelekezwa kwa Marekani. Katika maombi ya hivi punde zaidi, Waziri Mkuu wa Uhispania amesema katika mkutano na Papa Francis kuwa: "Ninaamini kuwa hatua ya jamii ya kimataifa ya kusitisha mchakato wa kuiuzia silaha Israeli ni ya dharura na muhimu sana kwa kuzingatia matukio yote yanayotokea katika eneo la Asia Magharibi." Matakwa kama haya yaliwasilishwa huko nyuma hata hivyo hayakutekelezwa, na bila shaka ipo haja ya kuitishwa mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuchunguza na kupasishwa matakwa hayo.