Kundi la Umoja wa Mataifa: Israel ilikiuka sheria za kimataifa katika hujuma dhidi ya Iran
(last modified Thu, 31 Oct 2024 11:35:03 GMT )
Oct 31, 2024 11:35 UTC
  • Kundi la Umoja wa Mataifa: Israel ilikiuka sheria za kimataifa katika hujuma dhidi ya Iran

Kundi la Marafiki Wanaotetea Hati ya Umoja wa Mataifa limesema hujuma ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran ilikuwa ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa na mipaka ya Iran.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, kundi hilo lenye wanachama 18 wa Umoja wa Mataifa limelaani vikali kitendo cha utawala wa Israel "kilichoratibiwa na cha kikatili" cha uchokozi dhidi ya Iran tarehe 26 Oktoba, ambacho kilipelekea kuuawa shahidi wanajeshi wanne wa Jeshi la Iran.

Ikumbukwe kuwa katika siku iliyotajwa, ndege za kivita za Israel zilitumia anga inayodhibitiwa na Marekani nchini Iraq kuvurumisha makombora kwenye vituo vya kijeshi katika majimbo ya Tehran, Khuzestan na Ilam nchini Iran na hivyo kukiuka mipaka ya nchi hii.

Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran ilithibitisha katika taarifa kwamba Israel ilitumia anga inayodhibitiwa na Marekani nchini Iraq katika kuishambulia Iran lakini pamoja na hayo mfumo wa ulinzi wa anga nchini uliweza kutungua aghalabu ya makombora hayo. Iran imesema imeazimia kujibu kitendo hicho cha uchokozi na haitaacha haki yake hiyo ya kulipiza kisasi.

Kundi hilo la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu kuendelea njama za utawala wa Israel za kuzusha vita vipana zaidi katika eneo la Asia Magharibi.

Kundi la Marafiki Wanaotetea Mkataba wa Umoja wa Mataifa lilianzishwa mnamo Julai 2021 huko New York na nchi 16 za awali ambazo ni Algeria, Angola, Belarus, Bolivia, Cambodia, China, Cuba, Korea Kaskazini, Eritrea, Iran, Laos, Nicaragua, Russia, Saint Vincent na Grenadines, Syria, na Venezuela na Palestina ambayo ni mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Mataifa.

Equatorial Guinea, Zimbabwe na Mali baadaye zilijiunga na kundi hilo huku Burundi, Ethiopia, Namibia, Afrika Kusini na Vietnam zikipewa hadhi ya waangalizi mwaka 2022.

Lengo kuu la kudi hilo ni kuunga mkono Hati ya Umoja wa Mataifa na kutumika kama jukwaa la kuhimiza kutumika sheria badala ya mabavu.