Adhanom: Ufadhili wa afya duniani unakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi kuwahi kutokea
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ameonya kuwa afya ya kimataifa iko hatarini huku msaada wa wafadhili ukikatika na WHO ikikabiliana na nakisi kubwa ya bajeti.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema kwamba shirika hilo linakabiliwa na "tatizo kubwa zaidi la ufadhili wa afya duniani" huku michango ikipungua kwa kasi katika nyanja zote.
Mgogoro huo umeongezeka zaidi baada ya Merekani kujiondoa kwenye shirika hilo Januari mwaka huu, ikidai kwamba WHO imeshughulikia vibaya janga la COVID-19 na majanga mengine ya kiafya ya kimataifa.
WHO imerekebisha mipango yake ya kifedha, kupunguza matumizi yake ya sasa na kupendekeza kupunguzwa kwa asilimia 21 ya bajeti ya 2026-2027.
"Bila shaka ni jambo chungu sana," amsema Tedros akionya kwamba kupunguzwa kwa bajeti kutaathiri moja kwa moja mifumo ya huduma ya afya duniani kote, haswa katika nchi zilizo hatarini zaidi.
WHO inapanga kupunguza viwango vyote vya shughuli zake, ikiwa ni pamoja na katika makao makuu yake huko Geneva na ofisi za kikanda na nchi. Baadhi ya ofisi katika mataifa tajiri huenda zikafungwa kabisa.