Putin: Tunatumai hatutalazimika kutumia silaha za nyuklia Ukraine
Rais wa Russia, Vladimir Putin amesema kufikia sasa, udharura wa kutumia silaha za nyuklia nchini Ukraine haujajitokeza, na kwamba anatumai hautatokea.
Katika kidokezo cha mahojiano yajayo na runinga ya serikali ya Russia, kilichorushwa hewani jana Jumapili na kusambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Putin alisema Russia ina nguvu na njia za kuhitimisha mzozo wa Ukraine kwa mantiki.
Akijibu swali kuhusu mashambulizi ya Ukraine katika eneo la Russia, Putin alisema: "Hakujawa na haja ya kutumia silaha hizo (za nyuklia) ... na ninatumai hazitahitajika."
"Tuna nguvu za kutosha na njia za kuleta kile kilichoanzishwa mnamo 2022 kwa hitimisho la kimantiki, na kupata matokeo ambayo Russia inahitaji," amesema Rais Putin.
Ikumbukwe kuwa, Putin alitia saini doktrini iliyotazamwa upya ya silaha za nyuklia za Russia mnamo Novemba 2024, ikielezea hali zinazoiruhusu Russia kutumia bomu lake la atomiki, ambalo ndilo kubwa zaidi ulimwenguni.
Doktrini hiyo ilipunguza kiwango hitajika cha dharura ya matumizi ya silaha hizo, na kumpa Putin chaguo la kujibu hata shambulio la kawaida kwa kutumia silaha za nyuklia.
Hii ni katika hali ambayo, Rais wa Russia alisema hivi karibuni kuwa, yuko tayari kushiriki katika juhudi za kuleta amani nchini Ukraine, na mashauriano ya kina yanaendelea kati ya Moscow na Washington.