Kurudi nyuma Marekani katika vita ilivyoanzisha dhidi ya Yemen; matunda ya Muqawama wa Wayemen
(last modified Thu, 08 May 2025 02:23:20 GMT )
May 08, 2025 02:23 UTC
  • Kurudi nyuma Marekani katika vita ilivyoanzisha dhidi ya Yemen; matunda ya Muqawama wa Wayemen

Msemaji wa harakati ya Muqawama ya Ansarullah, Muhammad Abdul Salam amesema, Yemen haitaiacha Ghaza peke yake licha ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita, na kwamba Marekani ndiyo iliyoomba kusitishwa mapigano.

Kuhusiana na suala hilo, Abdul Salam amesema: "msimamo wa sasa wa Yemen unaonyesha uimara na uthabiti wetu. Ombi la kusitisha mapigano limetolewa na Marekani na limetufikia sisi kupitia Oman".
Msemaji wa Ansarullah ameongezea kwa kusema: "Israeli imekatishwa tamaa sana na msimamo wa Marekani, kwa sababu Marekani imejaribu kujiokoa kutoka kwenye kinamasi cha Yemen".
 
Amesema, kulengwa vituo vya kiraia vikiwemo viwanda vya saruji, vinu vya kuzalisha umeme, vyanzo vya maji na viwanja vya ndege, ni ishara tosha ya kushindwa adui na akasisitiza: "kuwalenga raia na vituo vya umma ni kushindwa dhahir shahir na hakuwezi kuzuia uungaji mkono wetu kwa Ghaza."
 
Katika mabadiliko ya ghafla na ya wazi kabisa ya msimamo, Marekani imetangaza usitishaji mapigano katika vita vya Yemen. CNN imemnukuu afisa wa kijeshi wa Marekani na kuripoti kuwa, siku ya Jumatatu usiku, jeshi la nchi hiyo liliamriwa kusitisha mashambulizi dhidi ya Wahouthi (Ansarullah ya Yemen).
Trump

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutangaza kusitisha mashambulizi dhidi ya Yemen. Katika kauli aliyotoa Ikulu ya White House, Trump alimuamuru waziri wa mambo ya nje Marco Rubio na mshauri wake wa usalama wa taifa "wawajulishe watu wote kuhusu makubaliano hayo." Naye Rubio akayaelezea maafikiano hayo kuwa ni "mabadiliko muhimu."

 
CNN vilevile imeandika: duru za kuaminika zimetangaza kuwa, katika kipindi cha wiki iliyopita, Steve Witkoff, mjumbe maalumu wa Rais wa Marekani katika Mashariki ya Kati, ambaye anahusika na mazungumzo na Iran, amekuwa akifanya juhudi kwa ajili ya kusitisha mapigano na Wahouthi. Hatua hiyo inatathminiwa kama upigaji hatua moja mbele kuelekea kwenye mazungumzo yenye wigo mpana zaidi kati ya Marekani na Iran kwa lengo la kufikia mapatano ya nyuklia.
 
Mnamo Machi 15, Marekani ilianzisha mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Yemen yaliyoelezewa kama operesheni muhimu zaidi ya kijeshi kufanywa na Washington katika eneo la Asia Magharibi tangu Donald Trump arudi madarakani. Kwa kutoa amri rasmi katika tarehe hiyo, Trump aliidhinisha kufanywa mashambulizi ambayo yalikuwa yameshapangwa kwa wiki kadhaa. Katika mashambulizi hayo, maeneo tofauti ya Yemen yalipigwa mabomu na makombora mara mia kadhaa. Pentagon inadai kuwa imefanya zaidi ya mashambulizi elfu moja dhidi ya shabaha mbalimbali nchini Yemen. Katika operesheni hiyo, Marekani ilitumia ndege za kivita zilizokuwa kwenye manowari ya Harry Truman na Carl Vinson, pamoja na ndege za kivita za mashambulizi ya kimkakati aina ya B-2 zilizosheheni mabomu ya kuripua mahandaki ya GBU-57 yenye uzito wa tani 14.
 
Inavyoonekana, uamuzi wa Marekani wa kutangaza usitishaji vita umetokana na kushindwa Pentagon kuusambaratisha Muqawama wa Yemen na kuendelea mashambulizi ya makombora ya Yemen katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, sambamba na kuongezeka hasara inazopata Washington katika vita hivyo ilivyoanzisha dhidi ya Yemen. Baada ya mwezi mmoja na nusu tangu kuanza operesheni kubwa ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Yemen, vyombo vya habari vya nchi hiyo vimekiri kushindwa serikali ya Trump kufikia malengo yake.
Kuhusiana na hilo, CNN imeandika kuwa, kusitishwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Wahouthi kumefanyika katika hali ambayo, tangu ilipoanzishwa, operesheni hiyo ilikabiliwa na matatizo kadhaa. Kwa mujibu wa duru za habari, katika kipindi cha wiki saba tu, vikosi vya Ansarullah vimezidungua ndege saba zisizo na rubani za Marekani zenye thamani ya mamilioni ya dola, jambo ambalo limevuruga uwezo wa Washington wa kuingia katika "awamu ya pili" ya operesheni hiyo.
 
Sambamba na hayo, tarehe 22 Aprili, jarida la Foreign Policy, lilitoa makala yenye kichwa cha habari: "Vita vya Trump Dhidi ya Wahouthi Havifiki Popote," kuashiria kutokuwa na tija mashambulio ya Jeshi la Wanamaji la Marekani dhidi ya ngome za Ansarullah na likaandika: wiki tano baada ya Trump kushadidisha mashambulizi dhidi ya Yemen, matatizo kadhaa makubwa yamedhihirika, yakionyesha kuwa rais wa Marekani ana kibarua kigumu cha kuthibitisha madai yake kivitendo. Jarida hilo liliendelea kueleza: operesheni ya Marekani imeshindwa na kugonga mwamba katika kufikia malengo yake makuu mawili, ambayo ni kuhakikisha usalama wa vyombo vya baharini katika Bahari Nyekundu na kuzuia mashambulizi. Kiwango cha safari za majini katika Bahari Nyekundu na Mfereji wa Suez kingali ni cha chini mno, licha ya kuigharimu Marekani zaidi ya dola bilioni moja. Mkabala wake, majeshi ya Yemen yamezidisha mashambulizi yao dhidi ya Israel na meli za kivita za Marekani, mbali na kumtahadharisha Trump na hatari ya kutumbukia kwenye "kinamasi cha Yemen".
"Palestina 2", kombora la Hypersonic la Yemen linaloichachafya Israel

Ukweli ni kuwa, Marekani ilipuuza jambo moja muhimu katika mahesabu yake ya kijeshi; nalo ni uweledi wa wapiganaji wa Yemen na uzoefu wa miaka kadhaa waliopata katika vita vya kukabiliana na muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia. Vyombo vya habari vya Magharibi vilitoa taswira potofu kuhusu Wayemen kwa kuwaonyesha kuwa ni watu mabedui tu wasio na mifumo na miundo ya kijeshi, lakini matokeo ya operesheni za hivi karibuni yamethibitisha kuwa ukweli halisi uko kinyume na dai hilo. Kudunguliwa droni 27 aina ya MQ-9 Reaper na Muqawama wa Yemen ambako kumeitia Marekani hasara ya zaidi ya dola milioni 800 kunaonyesha kuwa, Wayemen sio tu wana ushujaa na ujasiri usioelezeka, lakini pia wana utaalamu wa kiufundi, umahiri wa kiwango cha juu, na zana zinazohitajika kwa ajili ya kutoa kipigo kwa adui.

 
Kushindwa kufikia malengo mashambulizi ya anga ya Marekani, ikiwemo kudhibiti nguvu za kijeshi za Yemen na hasara kubwa iliyopata Washington pamoja na kuendelea mashambulizi ya makombora ya Yemen dhidi ya Israel, yamemfanya hatimaye Trump alazimike kulegeza misimamo yake ya hapo awali na kutoa wito wa kusitishwa mapigano, ilhali kabla ya hapo alikuwa amedai kwamba anao uwezo wa kuipigisha magoti Yemen.../