Traore: Burkina Faso inataka ustawi wa kasi wa uhusiano na Russia
Rais wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, siku ya Jumamosi alisema anataka uhusiano wa nchi yake na Urusi ukue kwa kasi ya "kihistoria" na kupanuka katika maeneo mapya ya ushirikiano. Traore ametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wake na Rais wa Russia, Vladimir Putin, mjini Moscow.
Traore pia amesisitiza hitaji la msaada wa kiteknolojia na kubadilishana maarifa na Russia. Kwa upande wake, Putin ameeleza kuwa kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kinaendelea kukua, japo bado ni kidogo.
Amesema: "Tunahitaji kufanya kazi pamoja ili kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kupanua wigo wa biashara ya pande mbili." Rais wa Russia pia ametaja msaada wa kibinadamu unaoendelea kutolewa na Russia kwa Burkina Faso licha ya vikwazo vya kimataifa.
Amesema mwaka jana, Russia iliikabidhi Russia tani 25,000 za ngano bila malipo, na mwezi huu shehena kubwa ya bidhaa nyingine za chakula itawasili Ouagadougou.
Traoré, amezungumza kuhusu nafasi ya Russia kimataifa na kusema: "Licha ya vikwazo vyote vilivyowekwa dhidi ya Shirikisho la Russia na baadhi ya mataifa, Russia bado ina nafasi ya kipekee katika ulingo wa kimataifa, na sisi tunalizingatia hilo." Kiongozi huyo wa Afrika Magharibi aliwasili Moscow Mei 8 na alihudhuria Gwaride la Ushindi katika Uwanja wa Red Square siku iliyofuata, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 80 ya Ushindi katika Vita Vya Pili vya Dunia na Uzalendo.