Ripoti: Matajiri dunia wamesababisha theluthi mbili ya mabadiliko ya hali ya hewa
Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la Nature Climate Change umegundua kuwa asilimia 10 ya watu matajiri zaidi duniani wanahusika na theluthi mbili ya ongezeko la joto duniani linalooshuhudiwa tangu mwaka 1990, na athari mbaya uongezeo la mawimbi ya joto na ukame.
Utafiti pia umebaini kuwa 1% ya watu matajiri zaidi duniani wamechangia mara 26 ya wastani wa kimataifa wa ongezeko la kila mwezi la matukio mabaya ya hali ya hewa. Hii ina maana kwamba, mabadiliko ya hali ya hewa sio tu suala linalozihusu serikali, lakini pia linaweza kuhusishwa moja kwa moja na mtindo wa maisha wa watu na machaguo ya uwekezaji, ambavyo kwa upande wake vinahusishwa na utajiri.
Kwa mujibu wa utafiti huo, athari hizi za mabadiliko makali ya hali ya hewa ni mbaya zaidi katika maeneo hatarishi ya kitropiki, kama vile Amazon, Asia ya Kusini-Mashariki na Afrika Kusini, ambayo kihistoria yamekuwa na mchango mdogo zaidi katika uzalishaji wa hewa chafu duniani.
Matajiri huwa na mtindo wa maisha wa juu zaidi, na kila kitu wanachotumia au kununua huzalisha hewa ya kaboni. Kwa mfano, safari ya kibinafsi ya ndege ya tajiri mmoja hutoa kaboni dioksidi mara mia kadhaa zaidi ya ndege ya kibiashara.
Vilevile matajiri wengi ni wamiliki, wakurugenzi wakuu, au wanahisa wakuu wa makampuni yanayoendesha viwanda, kuchoma mafuta, au kukata misitu. Makampuni haya yanazingatia zaidi faida kuliko maendeleo endelevu, na wakati mwingine huchelewesha au kupinga kanuni za mabadiliko ya hali ya hewa ili kuepuka gharama.