Kwa nini nchi za Amerika ya Latini zimejiunga na safu ya wakosoaji wa Israel?
Rais Lula da Silva wa Brazil amesisitiza katika matamshi yake kwamba kinachoendelea Gaza si vita bali ni mauaji ya halaiki. Alifafanua: Tunachoshuhudia huko Gaza hivi sasa si vita kati ya majeshi mawili hata kidogo, bali kuna jeshi moja tu lenye weledi kamili ambalo linaua wanawake na watoto wa Ukanda wa Gaza.
Mwishoni mwa Februari 2024, Da Silva alisema katika taarifa yake kwamba, kinachofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza si vita bali ni mauaji ya halaiki, kwa sababu utawala huo unaua wanawake na watoto. Rais wa Brazil aidha amelaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza mapema katika taarifa yake na kusisitiza kuwa: Walimwengu hawapaswi kunyamaza kimya mbele ya mauaji yasiyoisha ya Israel dhidi ya Wapalestina.
Misimamo mikali ya Rais wa Brazil dhidi ya mauaji ya halaiki ya Wapalestina wakati wa vita vya Gaza ni moja ya kadhia za hivi karibuni za kuulaani utawala wa Kizayuni unaofanywa na wakuu wa nchi nyingi za Amerika ya Latini kutokana na jinai zisizo na idadi za utawala huo katika vita vya Gaza.
Nchi nyingi za Amerika ya Latini zimechukua misimamo mikali zaidi kati ya nchi zisizo za Kiislamu dhidi ya Israel na vitendo vyake vya jinai katika vita vya Gaza, na wakati huo huo, kwa kupunguza au kukata uhusiano na Tel Aviv na kuishtaki, pamoja na kuunga mkono mashtaka ya nchi nyinginezo kama vile Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za mauaji ya halaiki huko Gaza, zimeanzisha kampeni kubwa dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Venezuela ikiwa kinara wa nchi za kimapinduzi katika Amerika ya Latini, imekata uhusiano na Israel muda mrefu uliopita. Katika vita vya Israel na Lebanon mwaka 2006, Venezuela ilimwita nyumbani balozi wake kama ishara ya kupinga uvamizi wa Israel. Kwa upande mwingine, Tel Aviv pia ilimwita nyumbani mwakilishi wake kutoka Caracas na kwa muktadha huo uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande mbili ukawa umefikia tamati.
Kama ishara ya kupinga vita vya Gaza vya 2008-2009, serikali ya Venezuela ilikata uhusiano wote wa kisiasa na kiuchumi na Israel kwa wakati mmoja. Caracas daima imekuwa na misimamo imara dhidi ya utawala wa Kizayuni na kulaani vitendo vyake dhidi ya Palestina.
Kwa mfano, baada ya kufichuliwa jinai zilizofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wakati wa vita vya Gaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela, Ivan Khel Pinto, alitangaza uungaji mkono wa nchi yake kufuunguliwa mashtaka watenda jinai wa Israel mwishoni mwa Februari 2024 na kusema: "Ni muhimu jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kumuadhibu mvamizi na mtekelezaji wa mauaji ya halaiki."
Mwishoni mwa Oktoba 2023, baada ya uamuzi thabiti wa Bolivia wa kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni, wakuu mbalimbali wa mataifa ya Amerika ya Latini, zikiwemo Colombia, Brazil, Chile na Venezuela, pia walitoa radiamali kwa shambulizi la kulipuliwa kwa kambi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza na kukazungumziwa uuwezekano wa mataifa mengine kuchukua hatua kama ilivyochukluliwa na Bolivia.
Haukupita muda mrefu, Marais wa Colombia na Chile, Gustavo Petro na Gabriel Burich, waliwaita nyumbani mabalozi wao wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu wakilalamikia mashambulizi makubwa ya kijeshi ya Israel dhidi ya Gaza kwa lengo la kutathmini umuhimu wa kudumisha mazungumzo ya kidiplomasia na utawala wa Kizayuni.
Rais wa Chile, Gabriel Burich, alitangaza kwenye akaunti yake ya X: Chile inalaani vikali vitendo vya Israel na inaangalia kwa wasiwasi mkubwa operesheni hii ya kijeshi, ambayo iko katika awamu ya adhabu ya pamoja ya raia wa Palestina huko Gaza na haiheshimu kanuni za msingi za sheria za kimataifa.

Baadhi ya nchi za Amerika ya Latini zimekwenda mbali zaidi na kuchukua hatua dhidi ya utawala wa Kizayuni. Pamoja na mambo mengine, serikali ya Nicaragua ilitoa taarifa ikielezea uuzaji wa silaha za Ujerumani kwa Israel kuwa ni sawa na uhalifu wa kivita na ushiriki wa Ujerumani katika jinai za Israel na kutaka kukomeshwa hilo.
Nchi hii ya Amerika ya Kati iliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki mapema Machi 2024 na kuwataka majaji wa mahakama hiyo kutoa maagizo ya dharura ya kuzuia Berlin kutuma silaha na misaada mingine kwa Israel.
Rais Gustavo Petro wa Colombia pia alisema tarehe 1 Mei 2024 katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi, kwamba uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hiyo na utawala wa Kizayuni utakatika kabisa kutokana na jinai za utawala huu wa Gaza. Hatua ya Colombia ya kukata uhusiano na utawala wa Kizayuni lilikuwa pigo jingine kwa utawala huo na ilionekana kuwa ni hatua ya kuitenga zaidi Tel Aviv katika ngazi ya kimataifa.
Kimsingi, tangu kuanza kwa vita vya Gaza mwishoni mwa Oktoba 2023, nchi za Amerika ya Latini zimechukua misimamo hasi dhidi ya vitendo vya jinai vya Israel katika Ukanda wa Gaza hususan mauaji ya kimbari ya Wapalestina na utumiaji silaha za njaa na kuibua njaa katika eneo hilo, na sambamba na kulaani vitendo hivyo, zimekata na kupunguza uhusiano wao na utawala huo ghasibu wa Kizayuni na hata kuwasilisha malalamikp dhidi ya utawala huo wa Kizayuni katika asasi mahakama za kimataifa.