Kwa nini Marekani imewawekea vikwazo majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127326
Marekani mnamo Alhamisi, Juni 5, iliwawekea vikwazo majaji wanne wa kike wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa kushughulikia kesi zinazohusiana na Israel na hatua za Marekani nchini Afghanistan. Vikwazo hivyo, ambavyo mara nyingi huwekewa maafisa kutoka nchi zinazopinga Marekani, sasa vimewalenga maafisa wa mahakama ya kimataifa.
(last modified 2025-06-08T06:45:56+00:00 )
Jun 08, 2025 06:45 UTC
  • Kwa nini Marekani imewawekea vikwazo majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai?

Marekani mnamo Alhamisi, Juni 5, iliwawekea vikwazo majaji wanne wa kike wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa kushughulikia kesi zinazohusiana na Israel na hatua za Marekani nchini Afghanistan. Vikwazo hivyo, ambavyo mara nyingi huwekewa maafisa kutoka nchi zinazopinga Marekani, sasa vimewalenga maafisa wa mahakama ya kimataifa.

Vikwazo hivi vinafuatia kutolewa kwa hati za kukamatwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu na Yoav Gallant, Waziri wa zamani wa Vita wa Israel kwa kufanya jinai katika Vita vya Gaza. Majaji hao pia wamehusika katika kesi zinazohusu jinai za Marekani nchini Afghanistan. Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema katika taarifa kwamba Marekani itachukua hatua zozote zinazohitajika kwa ajili ya kulinda mamlaka yake, ya Israel na ya washirika wake wengine dhidi ya kile amekitaja kuwa "hatua zisizo halali za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai." Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, majaji hao wanne wamepigwa marufuku kuingia Marekani na mali yoyote ambayo huenda wakawa nayo nchini humo itazuiliwa.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imelaani hatua hiyo ikiitaja kuwa hatua ya kisiasa na kusema ni "jaribio la wazi la kudhoofisha uhuru wa taasisi ya mahakama inayoungwa mkono na nchi 125 duniani."

Betty Haller wa Slovenia na Reine Alapini-Gansou wa Benin walikuwa majaji wawili katika mahakama ambao walishiriki katika mchakato wa kutoa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant Novemba mwaka jana. Hati hiyo ilitolewa kwa sababu ya kuwawajibisha Netanyahu na Gallant kutokana na jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu na matumizi ya njaa kama silaha ya vita katika vita vya Gaza.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC

Majaji wengine wawili wa mahakama hiyo, Luz del Carmen Ibáñez Carranza wa Peru na Solome Balungi Bossa wa Uganda, pia wamewekewa vikwazo kwa kuhusika kwao katika kesi iliyoko mahakamani iliyopelekea kuidhinishwa kwa uchunguzi wa uwezekano wa jinai za kivita dhidi ya majeshi ya Marekani nchini Afghanistan.

Utawala wa Kizayuni na Marekani muungaji mkono wake mkuu walishangazwa na kushtushwa na hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya kutoa hati za kukamatwa maafisa wa ngazi za juu wa Israel na kukabiliana vikali na hatua hiyo. Ijapokuwa jinai za utawala wa Kizayuni hususan mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza na vile vile utumiaji njaa kama silaha ya vita ni jinai ambayo inaoonekana wazi huko Gaza, lakini Marekani imefanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuzuia jinai za utawala huo kuchunguzwa na taasisi za kimataifa kama vile Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Katika kujibu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Rais Donald Trump wa Marekani alitia saini amri ya utendaji mnamo Februari 6, 2025, akiidhinisha vikwazo dhidi ya mahakama hiyo kwa kile alikitaja "vitendo haramu na unyanyasaji wake dhidi ya Marekani na washirika wake, ikiwa ni pamoja na Israel." Kwa mujibu wa amri hiyo, "Marekani itawasababishia madhara makubwa wale wote wanaohusika na ukiukaji wa sheria katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ambayo baadhi yake yanaweza kujumuisha kufungiwa mali, pamoja na kusimamisha kuingia Marekani kwa maafisa, wafanyakazi na mawakilishi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, pamoja na wanafamilia wao wa karibu, kwa sababu kuingia kwao nchini Marekani kutakuwa na madhara kwa Marekani."

Katika agizo hilo, Trump alidai kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai haina mamlaka juu ya Marekani au Israel, kwani si wanachama wa Mkataba wa Roma wala Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Marekani inadai kuwa pande hizo mbili "zina demokrasia zinazositawi zenye wanajeshi ambao hufuata kikamilifu sheria za vita." Taarifa ya serikali ya Marekani kuhusu suala hili inasema: "Ukiukaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni pamoja na kuanzisha uchunguzi dhidi ya wafanyakazi wa Marekani na washirika wake, ikiwa ni pamoja na Israel.

Yoav Gallant (kushoto) na Netanyahu

Hatua ya Trump kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imekumbana na hisia hasi za kimataifa. Nchi 79 zikiwemo Canada, Ujerumani, Ufaransa, Afrika Kusini na Mexico, zimetoa taarifa ya pamoja zikipinga hatua ya Donald Trump kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, na kusema inadhoofisha utawala wa sheria za kimataifa.

Kimsingi, Trump ana mtazamo wa dharau kuhusu taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, na huzikubali pale tu utendaji wao unapoendana na maslahi ya Marekani na washirika wake duniani. Mfano wa wazi wa hili ni hati ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai iliyotolewa kwa ajili ya kukamatwa Rais Vladimir Putin wa Russia, ambayo ilikaribishwa na Washington na washirika wake.

Wakati huo huo, Marekani imechukua msimamo mkali dhidi ya mahakama hiyo hiyo, kwa kuwawekea vikwazo majaji wake, ambapo imetoa hati za kukamatwa kwa Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu na Gallant, Waziri wa zamani wa Vita wa Israel, na pia inapanga kuchunguza uhalifu wa askari wa Marekani nchini Afghanistan. Hata hivyo, radiamali ya kimataifa kwa hili inaonyesha kuwa licha ya hatua za upande mmoja za Marekani katika kuiunga mkono Israel, lakini nchi hiyo imepoteza heshima na itibari yake ya kimataifa, ambapo nchi nyingi duniani, hata washirika wa karibu wa Washington, sasa haziko tayari tena kukubali au kufuata kibubusa hatua hizo za upande mmoja na haramu hususan katika kipindi cha uongozi wa Trump.