Elon Musk atangaza kuanzishwa "American Party", asema: Marekani inaishi katika mfumo wa chama kimoja
-
Elon Musk
Bilionea wa Marekani, Elon Musk, alitangaza jana Jumamosi kuundwa kwa "American Party," siku moja baada ya kuandika chapisho kwenye jukwaa la X akiwauliza wafuasi wake ikiwa chama kipya cha siasa kinapaswa kuanzishwa nchini Marekani.
Musk amesema, "Kwa tofauti ya watu wawili kwa mmoja, mnataka chama kipya cha siasa, na mtapata." Ameendelea kuandika: "Leo, Chama cha Amerika kimeundwa ili kukurejeshea uhuru wako."
Tangazo la bilionea Elon Musk la luanzisha chama kipya cha siasa huko Marekani limetolewa siku moja baada ya Rais Donald Trump kutia saini muswada wa kupunguza ushuru, ambao Musk, mshirika wa zamani wa Trump, aliupinga vikali.
Musk alifadhili sehemu kubwa ya kampeni ya urais ya Trump na baadaye aliteuliwa kuwa mshauri mkuu wa rais. Aliongoza juhudi pana na zenye utata za kupunguza nguvu kazi na matumizi ya shirikisho kabla ya kung'atuka mwezi Mei mwaka huu.
Mwezi uliopita, tofauti kati ya Trump na Musk ziliongezeka na kudhihirika waziwazi, baada ya ushirikiano wa karibu kati ya watu wawili hao.
Wiki iliyopita, Trump alitishia kupunguza mabilioni ya dola katika ruzuku ya serikali ya shirikisho kwa kampuni za Musk.