Unajua kwa nini Marekani imemuwekea vikwazo Ripota Maalumu wa UN kuhusu Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu?
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, alitangaza Jumatano, Julai 9, kwamba atamuwekea vikwazo Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu, kwa kile alichokiita "juhudi zisizo halali zinazohusiana na uchunguzi wake kuhusu vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza" na eti kwa kuchukua "hatua dhidi ya maafisa wa Marekani na Israel."
Rubio amesema atamuwekea vikwazo Albanese "kwa juhudi zake zisizo halali na za kuaibisha za kuilazimisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuchukua hatua dhidi ya maafisa, makampuni na watendaji wa Marekani na Israel." Amesema: “Kampeni ya vita vya kisiasa na kiuchumi ya Albanese dhidi ya Marekani na Israel haitavumiliwa tena. Daima tutasimama na washirika wetu katika haki yao ya kujilinda."
Tovuti ya habari ya Washington Free Beacon imeripoti kuwa utawala wa Donald Trump umeutaka rasmi Umoja wa Mataifa kumfukuza kazi Francesca Albanese, ukimtuhumu kuwa "ana chuki dhidi ya Wayahudi na anaunga mkono ugaidi"!
Francesca Albanese, wiki hii alizikosoa nchi zilizomruhusu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuruka juu ya anga yao akielekea Marekani, akisema huenda zimekiuka wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. Ametahadharisha kuwa: "Mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza hayatakoma kwa sababu yanawanufaisha baadhi ya watu."
Mwanasheria huyu wa Kiitaliano, ambaye hapo awali alikabiliwa na mashambulizi mengi kutokana na msisitizo wake kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel umetenda jinai kubwa, ameinua juu kiwango cha maonyo yake katika ripoti yake ya hivi karibuni na kusisitiza kwamba: Kinachotokea hivi saa katika Ukanda wa Gaza si matokeo ya unyanyasaji wa kikoloni pekee, bali pia kina mizizi katika maslahi ya kiuchumi yaliyopangwa ambayo yanafaidika kwa utaratibu na maafa haya ya binadamu.
Hapo awali Ripota huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa aliutuhumu utawala wa Israel kwa kutumia vibaya lugha ya misaada ya kibinadamu kwa makusudi kwa ajili ya kuwezesha utekelezwaji wa jinai za kinyama huko Gaza na kusema: "Israel inajifanya kuhubiri masuluhisho ya kibinadamu ili kudumisha udhibiti wake huko Gaza na kuwanyima misaada muhimu ya kibinadamu watu wanaoteseka kwa njaa katika eneo hilo. Francesca Albanese amesisitiza kuwa: "Huu ni mkakati wa makusudi unaolenga kuficha uhalifu, kuwalazimisha watu kuwa wakimbizi, kuwalipua kwa mabomu, kuwachoma moto Wapalestina wakiwa hai, na kuwatia vilema manusura."
Msimamo huu imara wa afisa huyu wa Umoja wa Mataifa umewakasirisha viongozi wa Marekani na kuamua kumuwekea vikwazo kwa kutumia madai yaliyopitwa na wakati na ya uongo ya eti kwamba "ana chuki dhidi ya Mayahudi"