Uhispania na Ireland kujiunga na nchi zaidi ya 20 zitakazochukua 'hatua madhubuti' dhidi ya Israel
Uhispania na Ireland zitajiunga na zaidi ya nchi 20 zitazokutana katika mji mkuu wa Colombia, Bogota wiki ijayo kutangaza "hatua madhubuti" dhidi ya ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel.
Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, "mkutano wa dharura" unatazamiwa kufanyika mjini Bogota tarehe 15 hadi 16 Julai, ukisimamiwa na serikali za Colombia na Afrika Kusini kama wenyeviti wenza wa Kundi la The Hague, kuratibu hatua za kidiplomasia na za kisheria kukabiliana na kile wanachokielezea kuwa ni "hali ya kinga ya kutoadhibiwa" inayowezeshwa na Israel na washirika wake wenye nguvu.
Kundi la The Hague ni kambi ya mataifa manane kwa sasa, iliyozinduliwa tarehe 31 Januari katika mji huo wa Uholanzi kwa lengo la kuuwajibisha utawala wa kizayuni wa Israel kulingana na sheria za kimataifa.
"Kuundwa kwa Kundi la The Hague mwezi Januari kuliashiria hatua ya mabadiliko katika mwitikio wa kimataifa kwa ubaguzi na mmomonyoko mkubwa wa sheria za kimataifa," ameeleza Roland Lamola, waziri wa uhusiano wa kimataifa na ushirikiano wa Afrika Kusini.
"Moyo huohuo utahuisha mkutano huu wa Bogota, ambapo mataifa yatakayokusanyika yatatuma ujumbe wazi: hakuna taifa lililo juu ya sheria, na hakuna uhalifu utakaoachwa bila kujibiwa", amesisitiza Lamola.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amefafanua kuwa, kwa pamoja, nchi hizo zitashirikiana kuchukua hatua madhubuti za kisheria, kidiplomasia na kiuchumi ambazo zitaweza kukomesha haraka uharibifu unaofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Wanachama waanzilishi wa kundi hilo ni pamoja na Bolivia, Colombia, Cuba, Honduras, Malaysia, Namibia, Senegal na Afrika Kusini.
Mataifa yanayotarajiwa kushiriki katika mkutano huo ni pamoja na Algeria, Bangladesh, Bolivia, Brazil, Chile, China, Cuba, Djibouti, Honduras, Indonesia, Ireland, Lebanon, Malaysia, Namibia, Nicaragua, Oman, Ureno, Uhispania, Qatar, Uturuki, Saint Vincent na Grenadines, Uruguay, na Palestina.../