Polisi UK yakamata makumi ya watu kwa kushiriki maandamano ya kuiunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128270-polisi_uk_yakamata_makumi_ya_watu_kwa_kushiriki_maandamano_ya_kuiunga_mkono_palestina
Polisi wa Uingereza imewakamata makumi ya wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina wakati wa maandamano mapya ya kupinga marufuku ya vuguvugu la 'Palestine Action', kundi linalojulikana kwa maandamano yake dhidi ya makampuni ya silaha yenye uhusiano na Israel.
(last modified 2025-07-13T03:50:28+00:00 )
Jul 13, 2025 03:36 UTC
  • Polisi UK yakamata makumi ya watu kwa kushiriki maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Polisi wa Uingereza imewakamata makumi ya wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina wakati wa maandamano mapya ya kupinga marufuku ya vuguvugu la 'Palestine Action', kundi linalojulikana kwa maandamano yake dhidi ya makampuni ya silaha yenye uhusiano na Israel.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, Polisi ya Metropolitan walithibitisha kuwa watu 46 wamekamatwa baada ya wanaharakati kukusanyika kwenye uwanja wa Bunge jana Jumamosi, kwa wiki ya pili mfululizo, kupinga marufuku ya kundi hilo linaloipinga Israel.

Polisi walidai kuwa walikuwa wameonya wazi kwamba, kuunga mkono vuguvugu la 'Palestine Action' ni kosa la jinai baada ya maandamano kama hayo mwishoni mwa juma lililopita kusababisha watu 29 kukamatwa.

Kikundi cha 'Defend Our Juries' kilikuwa kimeandaa maandamano hayo, ambayo yalishuhudia vikundi viwili vidogo vikiketi pambizoni mwa masanamu ya Mahatma Gandhi na Nelson Mandela katika viwanja vya Bunge, wakiwa wamebeba bendera za Palestina na kupiga nara za kupinga mauaji ya kimbari.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na ujumbe unaosema, "Ninapinga mauaji ya halaiki, naunga mkono vuguvugu la Palestine Action.

Mbinyo huo wa polisi dhidi ya waandamanaji unajiri katika hali ambayo, takriban wabunge 60 wa Uingereza hivi karibuni waliitaka serikali ya London kulitambua rasmi taifa la Palestina, kufuatia mpango tata wa Israel wa kuwahamisha kwa nguvu wakazi wa Gaza na kuwapeleka Rafah.