Karibu 50% ya Wajapan manusura wa bomu la nyuklia wasema "hawawezi kuisamehe" Marekani
Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Habari la Kyodo la Japan unaonyesha kuwa, karibu asilimia 70 ya manusura wa shambulio la bomu la atomiki lililofanywa na Marekani dhidi ya nchi hiyo wanaamini kuwa silaha za nyuklia zinaweza kutumika tena.
Manusura hao wametolea mfano wa mvutano unaoongezeka duniani, ikiwa ni pamoja na vita vya Russia na Ukraine na uundaji wa silaha hizo unaofanywa na Korea Kaskazini.
Uchunguzi huo umefanywa sambamba na kukaribia maadhimisho ya miaka 80 tangu silaha za nyuklia zilipotumiwa kwa mara ya kwanza na Marekani wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Manusura 1,500 wa shambulio hilo walishiriki katika uchunguzi huo, huku 68.6% wakisema hatari ya silaha za nyuklia kutumika tena inaongezeka.
45.7% ya waliohojiwa walisema "hawawezi kuisamehe" Marekani kwa mashambulizi hayo ya mabomu yaliyoteketeza roho za raia wasio na hatia, wakati 24.3% walisema "hawana hisia maalumu" na 16.9% walisema "hawajui."
Mwaka huu unasadifiana na kumbukumbu ya miaka 80 tangu Marekani ilipodondosha mabomu ya atomiki huko Hiroshima na Nagasaki magharibi mwa Japan karibu na mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia.
Mnamo Agosti 6, 1945, Marekani ilidondosha bomu la atomiki katika mji wa Hiroshima, na kuua takriban watu 140,000.
Bomu la pili lilidondoshwa mjini Nagasaki siku tatu baadaye, na kusababisha vifo vya watu wengine 70,000.../