Kupungua uungaji mkono wa wafuasi wa MAGA kwa vita vya Israel dhidi ya Iran; sababu, matokeo na athari zake kwa siasa za Marekani
Katika miezi ya hivi karibuni, anga ya kisiasa ya Marekani imeshuhudia mabadiliko makubwa katika mtazamo wa wafuasi wa MAGA yenye maana ya Ifanye Tena Kuu Marekani, (Make America Great Again) kuhusiana na vita vya Israel dhidi ya Iran.
Japokuwa mwanozoni kundi hili liliunga mkono mashambulizi ya Israel kwa shauku kubwa, lakini uchunguzi mpya wa maoni unaonyesha kuwa uungaji mkono huo umepungua.
Mabadiliko hayo ya kimtazamo yanaweza kuwa na taathira kubwa kwa sera za utawala wa Donald Trump na juu ya matokeo ya uchaguzi ujao nchini Marekani.
Uchunguzi wa maoni ambao ulifanywa na taasisi ya J.L. Partners mwishoni mwa msimu wa machipuo mwaka huu ulionyesha kuwa karibu 65% ya wafuasi wa MAGA wanaunga mkono mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran. Aidha, uchunguzi mwingine wa maoni uliofanywa na Taasisi ya GrayHouse ulionyesha kuwa karibu 90% ya wafuasi wa Donald Trump wanakubaliana na uamuzi wa kufanywa mashambulizi ya kijeshi ya kiwango fulani dhidi ya Iran na wanalichukulia hilo kuwa ni hatua za uingiliaji kijeshi wenye mpaka maalumu na si vita kamili.
Tarakimu hizi zilionyesha kuwepo uungaji mkono mkubwa kwa msimamo wa washupaliaji vita kwa kisingizio cha tishio la nyuklia la Iran.
Hata hivyo, mwenendo huo wa uungaji mkono umebadilika katika miezi ya hivi karibuni. Uchunguzi wa maoni uliofanywa kwa pamoja na jarida la Economist na taasisi ya YouGov katika msimu wa kiangazi umebaini kuwa ni asilimia 23 tu ya Warepublican wanaamini kuwa ni lazima Marekani iingilie moja kwa moja mzozo kati ya Iran na Israel, wakati asilimia 60 wamepinga msimamo huo. Ripoti nyingine iliyotolewa na gazeti la The Daily Beast imeonyesha kuwa asilimia 53 ya wafuasi wa
Trump wamepinga Marekani kujiunga na Israel katika kuishambulia kijeshi Iran.
Kupungua uungaji mkono huo kunapasa kuzingatiwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika miezi iliyopita, ambapo akthari ya wafuasi wa Trump walikuwa wakiunga mkono sera za hujuma na uvamizi wa kijeshi. Hii inaonyesha kuwa, mitazamo ya wafuasi hao, sasa imekuwa ya kihafidhina na ya tahadhari zaidi.
Kuna mambo kadhaa ambayo yamechangia mabadiliko hayo ya kimtazamo.
Kwanza ni wasiwasi kuhusu vita vya muda mrefu na gharama zake. Wafuasi wa MAGA, ambao kijadi wanatilia mkazo kauli mbiu ya "Marekani Kwanza" na kujiepusha na vita vya nje ya nchi wana wasiwasi kwamba vita vya moja kwa moja vya Marekani na Iran vinaweza kusababisha mzozo wa muda mrefu na wenye gharama kubwa. Kumbukumbu za vita vilivyogonga mwamba huko Afghanistan na Iraq, vilivyoandamana na kupanda kwa bei ya nishati na makali ya kiuchumi, vimekuwa sababu ya wafuasi hao wa “Marekani Kwanza” kuwa wapizani wakali wa uingiliaji mpya wa kijeshi.
Jambo la pili ni kuwepo mgongano na kauli mbiu "Amerika Kwanza". Sera ya "Amerika Kwanza" ni mhimili mkuu wa itikadi ya MAGA, na sera hii inatilia mkazo kuzingatiwa kwanza maslahi ya ndani ya Marekani badala ya kujihusisha na migogoro ya nje ya nchi. Mzozo wa Asia Magharibi na gharama zake vinakinzana na kauli mbiu hiyo, na kwa sababu hiyo baadhi ya wafuasi wa MAGA wanaamini kwamba Marekani inapaswa kujiepusha na vita hivyo.
Na baada ya yote hayo kuna migawanyiko ya ndani katika uongozi wa MAGA. Baadhi ya viongozi wake akiwemo Marjorie Taylor Greene na Steve Bannon, wanapinga uingiliaji wa moja kwa moja wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran na wanataka Washington ijikite zaidi kwenye sera ya vikwazo na diplomasia. Tofauti hizo katika uongozi zimeathiri pia mtazamo wa wafuasi.
Kupungua uungaji mkono wa kambi kuu ya Trump kwa vita dhidi ya Iran ni changamoto kubwa kwake yeye na sera zake. Kwa upande mmoja, Trump anahitaji kulinda uungwaji mkono huo mkubwa anaopata kutoka kwa kundi hilo ili kushinda uchaguzi ujao; na kwa upande mwingine, maoni ya umma na ngome yake ya uungaji mkono vinamshinikiza aepukane na vita vya gharama kubwa.
Katika uchaguzi wa rais wa Marekani, kulinda uungaji mkono wa wafuasi wa MAGA ni jambo muhimu sana kwa Trump. Kwa sababu hiyo kupungua uungaji mkono wa vita vya Israel dhidi ya Iran kwa wafuasi wa MAGA kunaonyesha hali tata na ya mabadiliko inayojiri katika anga ya kisiasa ya Marekani. Mabadiliko hayo ya mtazamo ni muhimu, si kwa sera za nje tu, lakini pia kwa anga ya kisiasa ya ndani na kwa uchaguzi ujao wa nchi hiyo…/