Rais Maduro alaani kimya cha walimwengu kwa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina
Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amekosoa vikali kimya cha walimwengu mbele ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni na kusisitiza haki ya muqawama (mapambano) na kuwepo taifa la Palestina.
Akizungumza leo katika "Mkutano wa Bogotá" katika mji mkuu wa Colombia Maduro amesema: "Tunaonyesha hasira na kupaza zetu na sauti kwa uthabiti dhidi ya ukimya wa ulimwengu katika kukabiliana na mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina."
Rais wa Venezuela ameongeza kusema kuwa, "Tunachoshuhudia huko Gaza na Palestina nzima sio mzozo kati ya pande zinazovutana, bali ni mpango wa kimfumo wa kuwaangamiza watu na kutokomeza utambulisho wao."
Aidha Nicolas Maduro mmoja wa waungaji mkono wa Wapalestina amesema, "Kila bomu linalorushwa kwenye hospitali, shule au nyumba ya Wapalestina sio tu kwamba linaua watu wasio na hatia bali pia linaharibu misingi ya amani ya dunia."
Alisema: "Tunasisitiza kwamba Palestina ina haki ya kuwepo, kuendesha muqawama, na kuishi kwa uhuru katika nchi huru kikamilifu na Baytul-Muqaddas Mashariki kuwa mji mkuu wake."
"Mkutano wa Bogotá", ambao ni wa kwanza unafanyika kwa kushirikisha wanachama wa "Hague Group" na baadhi ya nchi nyingine, unatazamiwa kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na jinai za utawala wa Israel huko Gaza.
Kundi la The Hague lilianzishwa Januari 31 mwaka huu huko The Hague, Uholanzi, kwa ushiriki wa Bolivia, Cuba, Honduras, Senegal, Afrika Kusini, Malaysia, Namibia na Colombia.
Na Salum Bendera