Afisa wa zamani wa Pentagon: Huenda US ikaishiwa na makombora
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128476-afisa_wa_zamani_wa_pentagon_huenda_us_ikaishiwa_na_makombora
Mshauri wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), Douglas Macgregor ameonya kuwa, Marekani inaweza kuishiwa na hifadhi yake ya makombora ndani ya siku nane.
(last modified 2025-07-18T11:01:03+00:00 )
Jul 18, 2025 10:44 UTC
  • Afisa wa zamani wa Pentagon: Huenda US ikaishiwa na makombora

Mshauri wa zamani wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon), Douglas Macgregor ameonya kuwa, Marekani inaweza kuishiwa na hifadhi yake ya makombora ndani ya siku nane.

Macgregor ameeleza kuwa, Rais Donald Trump anapaswa kufahamishwa kuhusu jinsi hifadhi ya makombora ya Marekani "ilivyo tupu."

Shirika la habari la Sputnik limemnukuu Macgregor akiitaka Marekani "iache kutuma silaha nje ya nchi" huku akionya kuhusu hifadhi hafifu ya Marekani ya makombora ya kushambulia na kujihami.

"Hii inamaanisha kuwa, tunaweza kupigana vita vya siku 8, halafu tutalazimika kwenda kwenye nyuklia," mshauri huyo wa zamani wa Pentagon amebishana katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Matamshi hayo ya afisa wa zamani wa Pentagon yanajiri siku chache baada ya Rais Trump kutangaza kutuma shehena mpya kubwa za silaha za Marekani kuelekea Ukraine.

Russia imesisitiza mara kwa mara kuwa, silaha za masafa marefu zinazotolewa na nchi za Magharibi zinatumiwa na vikosi vya Ukraine kuwalenga raia katika ardhi ya Russia na kuvuruga juhudi za amani.

Kuruhusu Ukraine kutumia silaha hizi kutabadilisha kimsingi asili ya mzozo huo, kama Rais wa Russia, Vladimir Putin alivyosema hapo awali. "Tutafanya maamuzi muhimu kwa mujibu wa vitisho vinavyotukabili," alionya Putin karibuni.

"Swali kuu ni iwapo nchi wanachama wa NATO zichukuliwe kuwa zinahusika moja kwa moja katika mzozo wa kijeshi au la," Rais amehoji Rais wa Russia.