Sababu za Kundi la The Hague kusimamisha biashara ya kijeshi na utawala wa kizayuni
Nchi zinazounda Kundi la Hague, yaani The Hague Group zimetangaza kuwa zimesitisha biashara ya kijeshi na utawala wa kizayuni wa Israel.
Kundi la The Hague, ambalo linaunganisha nchi zipatazo 30 zinazolenga kuchukua "hatua zilizoratibiwa za kisheria na kidiplomasia" dhidi ya utawala wa kizayuni, limetangaza kusimamisha kufanya biashara ya silaha na vifaa vya kijeshi na utawala huo, pamoja na kupiga marufuku safari za meli zake. Taarifa ya pamoja iliyotolewa na kundi hilo siku ya Jumatano imesema: "tunatangaza hatua zifuatazo ... kuzuia utoaji au usafirishaji wa silaha, risasi, fueli ya kijeshi, vifaa vya kijeshi vinavyohusiana nayo, na vitu vyenye matumizi namna mbili kwa Israel ... kuzuia upitishaji, utiaji nanga na utoaji huduma kwa meli katika bandari yoyote ... kuzuia usafirishaji wa silaha, risasi, fueli ya kijeshi, vifaa vya kijeshi vinavyohusiana nayo na vifaa vyenye matumizi namna mbili kuelekea Israel kwa kutumia meli zinazopeperusha bendera zetu."
Baada ya kikao cha mawaziri wa nchi zinazounda Kundi la The Hague kilichofanyika mjini Bogota, Colombia, nchi hizo zilikubaliana kuzuia miamala kati ya mashirika ya serikali na utawala wa kizayuni wa Israel na "kuanzisha mapitio ya haraka ya mikataba yote ya umma ili kuzuia taasisi na mifuko ya fedha ya umma kuusaidia utawala haramu wa Israel katika kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na kuzuia kufanywa kuwa jambo la kawaida uwepo huo haramu wa Israel".
Hati hiyo ilitiwa saini na Bolivia, Cuba, Colombia, Indonesia, Iraq, Libya, Malaysia, Namibia, Nicaragua, Oman, Saint Vincent na Grenadines na Afrika Kusini. Muungano wa nchi hizo zilizokutan Bogota ulitangaza kuwa zitatoa mjibizo kwa jinai zinazofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel huko Ghaza, kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzuia kupelekewa silaha utawala huo. Mkutano wa siku mbili wa Bogota ulimalizika Jumatano kwa nchi 24 kukubaliana kuchukua hatua sita kwa madhumuni ya "kudhibiti mashambulio ya Israel dhidi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu."
Kundi la The Hague ni muungano wa nchi kutoka Kusini mwa Dunia (Global South) ambao uliundwa tarehe 31 Januari 2025 ili kutekeleza hukumu za Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuhusiana na mzozo wa Israel na Palestina. Kundi la The Hague awali liliundwa likiwa na nchi tisa wanachama. Mnamo tarehe 3 Aprili 2025, wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Maripota Maalumu Francesca Albanese, Telang Mfukong na Jovana Jedmirovic Ranito, walitoa wito kwa nchi zaidi kujiunga na Kundi la Hague, kwani walikuwa na wasiwasi kwamba kutochukuliwa hatua kutahatarisha mfumo wa sheria wa kimataifa. Kufuatia hatua hiyo, Kundi la The Hague lilitangaza kwamba litafanya mkutano wa dharura huko Bogotá tarehe 15-16 Julai 2025, ambapo nchi wanachama zitatangaza hatua maalumu na zilizoratibiwa za utekelezaji wa sheria za kimataifa. Ilitarajiwa, wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 20 wangehudhuria mkutano huo, zikiwemo Brazil, China, Indonesia, Ireland, Ureno, Qatar, Uhispania na Uturuki. Lakini zaidi ya nchi 30 zilihudhuria mkutano wa Bogota, zikiwemo pia Mexico, Norway na Pakistan. Idadi ya wanachama wa Kundi la The Hague inatarajiwa kuongezeka katika "miezi ijayo."
Hatua muhimu ya Kundi la The Hague ya kupiga marufuku biashara ya kijeshi na utawala wa Kizayuni ni hatua nyingine muhimu katika uga wa kuuwekea vikwazo vya silaha utawala huo na kutengwa zaidi kimataifa. Baada ya kuanza vita vya Ghaza kufuatia Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya tarehe 7 Oktoba 2023 na jinai zisizo na kifani zilizofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Ghaza hususan mauaji ya kimbari na utumiaji wa silaha ya njaa na kusababisha baa la njaa katika eneo hilo, ili kuongeza mashinikizo na kutengwa utawala wa Kizayuni, vuguvugu la kuususia utawala huo ghasibu katika upeo wa ulimwengu mzima limefikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa; na taasisi pamoja na nchi nyingi duniani zinataka utawala huo haramu uwekewe vikwazo vya silaha. Umoja wa Mataifa pia umetoa wito wa kuzidishwa ususiaji dhidi ya Israel kwa lengo la kuishinikiza ikomesha vita huko Ghaza.
Licha ya unga’nga’nizi wa washirika wakuu wa utawala wa Kizayuni yaani Marekani, Ujerumani na Uingereza wa kuendelea kuupelekea zana na silaha za kijeshi utawala huo, muelekeo wa kimataifa unafuata mkondo kinyume na huo ambao ni wa kushadidisha vikwazo dhidi ya Israel vikiwemo vya silaha na zana za kijeshi.../