Nadharia ya ulimwengu wa kambi kadhaa; mwelekeo huu utaimarishwa katika Mkutano wa Shanghai?
Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO) unaohudhuriwa na viongozi kutoka zaidi ya nchi 20 ulianza jana Jumapili katika mji wa Tianjin wa China.
Mkutano wa Shanghai unatazamiwa kuainisha dira ya muongo mmoja ujao kwa kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na kubuni mkakati wa maendeleo na ustawi wa jumuiya hiyo kwa mwaka 2035. Rais wa Russia, Vladimir Putin na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia watatia saini Azimio la Tianjin na Mkakati wa Maendeleo kwa Muongo Ujao.
Katika ulimwengu wa sasa, ambapo dunia inazidi kushuhudia ukosefu wa mtikisiko katika miundo ya awali ya kisiasa na kiuchumi, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai inaweza kutambuliwa kuwa moja ya taasisi muhimu zaidi za kimataifa za kikanda. Jumuiya hiyo iliyoanzishwa mwaka 2001, imetangaza kuwa lengo lake ni kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kiusalama na kiutamaduni kati ya nchi za Asia ya Kati, China na Russia. Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zikiongozwa na China na Russia, zinajaribu kuunda utaratibu mpya wa uhusiano wa kimataifa kwa kusisitiza msimamo na sera ya ulimwengu wa kambi kadhaa na kukabiliana na sera ya dunia ya kambi moja ya Magharibi.
Iran, ikiwa ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, pia inahudhuria mkutano huo ikiwakilishwa na Rais Masoud Pezeshkian aliyewali China jana Jumapili. Kabla ya safari hiyo, Pezeshkian alisema kuwa,Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai zinawakilisha karibu watu bilioni 2.5, na zinachangia zaidi ya asilimia 40 ya uchumi wa dunia. Alisisitiza kuwa: "Mkutano wa Shanghai ni fursa muhimu na mwafaka ya kuimarisha ushirikiano wa pande nyingi na mwingiliano wa kikanda."
Iran ambayo ina umuhimu mkubwa katika eneo la Asia Magharibi kutokana na nafasi yake mahususi ya kijiografia na kiuchumi, imeimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na China na Russia katika miaka ya hivi karibuni hususan katika nyanja za nishati na biashara, na sasa Mkutano wa Shanghai ni fursa nyingine ya kupanua uhusiano wa Iran na China na Russia katika nyanja nyinginezo, pamoja na nchi nyingine wanachama wa Shanghai.
Mkutano wa wakuu wa Shanghai unafanyika sambamba na ziara ya siku nne ya Rais Vladimir Putin wa Russia nchini China. Ziara hiyo sio tu tukio muhimu la kidiplomasia kwa Russia na China, lakini pia una umuhimu katika mtazamo wa matukio ya kimataifa na mchakato wa kubuni utaratibu mpya wa dunia. Putin ambaye amewasili China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping wa China kuhudhuria mkutano wa wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), atakutana na maafisa mbalimbali wa serikali ya China kando ya mkutano huo na kujadili masuala muhimu ya kikanda na kimataifa.
Mojawapo ya malengo muhimu ya wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai ni kuimarisha nafasi ya shirika hilo katika kukabiliana na changamoto za kimataifa, ikiwa ni pamoja na masuala ya jeopolitiki, hitilafu za kibiashara na kuyumba kwa uchumi.
Mkutano wa sasa wa Shanghai unafanyika katika wakati ambapo sera za Rais wa Marekani, Donald Trump, za kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, ikiwa ni pamoja na kutoza ushuru mkubwa wa kibiashara na kuweka vikwazo vya kiuchumi na kisiasa, umefanya hali ya kisiasa na kiuchumi kuwa ngumu kwa nchi nyingi duniani. Kwa hivyo, mkutano wa sasa wa wa SCO ni muhimu sana katika kupunguza athari za sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani kuhusu utaratibuu wa dunia na siasa za kimataifa.
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai zinasisitiza kwamba zinalenga kuunda utaratibu wa kimataifa unaotegemea ushirikiano wa pande nyingi. Kuhusiana na suala hilo, nchi zilizohudhuria mkutano huu, hasa China na Russia, zinasimama waziwazi kupinga juhudi za Magharibi za kubadili utaratibu wa kimataifa na kusisitiza umuhiimu wa kuundwa dunia yenye kambi kadhaa; mtazamo ambao, katika siasa za kimataifa, unaweza kuonekana kama changamoto kwa utawala wa kibeberu wa Marekani na madola mengine ya Magharibi.
Kwa upande mwingine, wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai pia wanakabiliwa na changamoto kadhaa. Miongoni mwa changamoto hizo ni migogoro ya ndani kati ya nchi wanachama wake. Pia, tofauti katika kiwango cha ustawi na maendeleo ya kiuchumi na mahitaji tofauti ya nchi wanachama vinaweza kuathiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja uwezo wao wa kufikia makubaliano ya pande zote na jumuishi. Masuala haya yanaonyesha kuwa licha ya irada na hamu ya nchi wanachama ya kukabiliana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za nchi za Magharibi na kuunda utaratibu mpya wa dunia, ufanisi wa malengo hayo kivitendo unaweza kukabiliwa na changamoto kubwa.
Pamoja na hayo inatupasa kusema kuwa, Mkutano wa Shanghai bado unaweza kutumika kama jukwaa muhimu la kubuni utaratibu mpya wa dunia na kukabiliana na sera za Magharibi za sera ya kambi moja. Hivyo basi, iwapo nchi wanachama zitaweza kushinda changamoto zao za ndani, jumuiya hiyo inaweza kuwa na nafasi na mchango muhimu katika kufafanua upya uhusiano wa kimataifa katika siku zijazo.