Kwa nini New Delhi imekhitari sera ya kuwa karibu zaidi na Tel Aviv?
-
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi
India na utawala wa Kizayuni wa Israel zimeanzisha uhusiano mkubwa baina ya pande hizo mbili katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa kuachana na sera yake ya muda mrefu katika kanda ya Asia, ambayo ilitokana na siasa za kuishi kwa amani na nchi za kikanda, hasa majirani zake, India imeanzisha uhusiano wa karibu na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika miaka ya hivi karibuni pia Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amefanya mikutano kadhaa na mwenzake wa Israel, Benjamin Netanyahu, na amefanya makubaliano makubwa ya kijeshi na biashara na Tel Aviv. Vilevile kumekuwepo mikutano mingi kati ya maafisa wakuu wa India na Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa'ar, mnamo Novemba 3, 2025 alikutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa India, S. Jaishankar, na Mshauri wa Usalama wa Taifa, Ajit Doval. Mazungumzo hayo yalilenga ushirikiano katika usalama wa kikanda na mpango wa amani wa Gaza, na pande zote mbili zilisisitiza sera inayoitwa "kutovumilia kabisa" ugaidi. Wakati huo, Gideon Sa'ar aliitaja India kuwa ni "nchi yenye nguvu duniani" na kusema, Israel inataka kuwa na "ushirikiano wa kimkakati wa muda mrefu" na India kwa msingi wa maadili ya pamoja ya kidemokrasia na malengo ya usalama wa pande mbili.
India inatambuliwa kuwa mnunuzi mkuu wa silaha kutoka kwa utawala wa Israel, ikichangia asilimia 43 ya jumla ya silaha zinazouzwa na utawala huo, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (SIPRI). Kwa ujumla, sera za India kuhusu suala la Palestina zimejaa utata na migongano, na sasa New Delhi imeacha kuwaunga mkono watu wa Palestina wanaoteseka kutokana na uvamizi na badala yake inautetea na kuuunga mkono wa utawala wa Kizayuni. Uungaji mkono huo hauishii katika nyanja za kisiasa na kiuchumi tu, bali hata unajumuisha masuala ya kijeshi. Swali linalojitokeza hapa ni kwamba hali hii imetokea vipi na kwa nini?
Mnamo 1947 India ilipiga kura dhidi ya kugawanywa Palestina katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na ilikuwa nchi ya kwanza isiyo ya Kiarabu kutambua rasmi Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kama mwakilishi pekee halali wa watu wa Palestina hapo mwaka 1974. Vilevile India ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza kutambua rasmi dola la Palestina mnamo 1988. Ingawa India iliutambua utawala wa Kizayuni mnamo 1950, lakini haikuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo hadi mwaka 1992.
Kinyume na hayo yote yaliyosemwa, serikali ya India ilitangaza uungaji mkono mkubwa wa kisiasa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel mara tu wanamapambano wa Palestina walipotekeleza Operesheni "Kimbunga cha Al-Aqsa" mnamo Oktoba 7, 2023. Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alikuwa kiongozi wa kwanza wa dunia kulaani Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa. Modi na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Subrahmanyam Jaishankar walidhihirisha msimamo huo huo, wakidai kwamba "ikiwa Misri haitakabiliana na itikadi kali, inaweza kukumbana na hatima hiyo hiyo." Katika fremu hiyo hiyo ya kuutetea na kuuunga mkono utawala katili wa Israel bila masharti wala mpaka, India ilikataa kupiga kura kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa lililotaka kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza kwa sababu za kibinadamu.
Uungaji mkono huo wa New Delhi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel uliathiri mitazamo ya Wahindu wenye msimamo mkali wa kitaifa, ambao walianzisha kampeni ya kusambaza taarifa za kupotosha kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kile kilichokuwa kikiendelea katika Ukanda wa Gaza, kwa niaba ya simulizi za utawala wa Kizayuni.
Ili kuelewa sababu za mabadiliko makubwa katika sera ya India kuhusiana na Palestina, uchambuzi mwingi unaonyesha mambo mawili ya msingi, ambayo ni:
Mosi, kupanuka utaifa wa Kihindu. Ashok Swain, Mkuu wa Idara ya Amani na Utafiti wa Migogoro katika Chuo Kikuu cha Uppsala nchini Sweden, anasema kwamba utaifa wa Kihindu umekuwa ukiongezeka tangu Modi awe Waziri Mkuu. Hata hivyo mtafiti huyo anaamini kwamba Wahindi wengi bado wanaunga mkono mapambano ya Wapalestina kwa ajili ya ukombozi na kujitawala. Inatupasa pia kusema kuwa, vyombo vya habari vya India vimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na serikali yenye misimamo mikali ya Kihindu; na kwa msingi huo huwa na mwelekeo wa kihasama zaidi dhidi ya Palestina.
Jambo la pili, ni uadui dhidi ya Uislamu. Ashok Swain anasema kwamba serikali ya Narendra Modi inaamini vyombo vya habari vya India vitailaani Hamas maadamu vita bado vinaendelea huko Gaza. Mbinu hii ni fursa ya kuzidisha chuki dhidi ya Uislamu ndani ya jamii ya India. Ashok Swain anaamini kwamba, kuna mambo mengi yanayokutanisha pamoja Uzayuni na Uhindu, na kwamba itikadi zote mbili zina malengo sawa ya kujitanua na kuwafutilia mbali wengine. Uzayuni na Uhindu zote mbili zinadai kwamba India na Palestina hapo awali zilikuwa tamaduni mbili za Kihindu na Kiyahudi, lakini zimechafuliwa na watu wa nje, haswa Waislamu, na kwa sasa pande zote mbili zinataka kurejesha eti utukufu wa zamani wa mataifa ya Kihindu na Kiyahudi!
Katika muktadha huu, gazeti la Ufaransa la Le Monde limeripoti kwamba baadhi ya Wahindu wenye msimamo mkali wametangaza utayarifu wao wa kubeba silaha pamoja na Wazayuni, na katika muktadha huu, Naor Gilon, balozi wa Israel nchini India, amejigamba kwamba anaweza kuunda jeshi la watu wa kujitolea wa Kihindu.