Mahakama ya Uturuki yatoa waranti wa kukamatwa Netanyahu kwa kutenda jinai Gaza
-
Mahakama ya Uturuki yatoa waranti wa kukamatwa Netanyahu kwa kutenda jinai Gaza
Mahakama ya Uturuki imetoa hati ya kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, waziri wake wa ulinzi na maafisa wengine 35 wakuu wa Israel kwa tuhuma za "uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari."
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Istanbul imesema hukumu hizo zinahusiana na vitendo vyao dhidi ya kundi la kimataifa ambalo lilikuwa likijaribu kutoa msaada kwa Wapalestina waliozingirwa na jinai dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Hatua hiyo inaashiria mojawapo ya changamoto kubwa za kimataifa za kisheria dhidi ya maafisa wa Israel kuhusiana na uhalifu wao wa kivita huko Gaza, na kuimarisha mahitaji ya kimataifa ya uwajibikaji huku kukiwa na madai ya mashambulizi ya kimfumo dhidi ya raia.
Maafisa 37 wa utawala ghasibu wa Israel wametajwa katika hati za kukamatwa, ingawa majina mengi bado hayajatolewa hadharani.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa Istanbul ilisema kuwa, mbali na Netanyahu washukiwa hao ni pamoja na Waziri wa Vita Israel Katz, Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir, na Mkuu wa Jeshi Lt. Jenerali Eyal Zamir.
Taarifa hiyo imeushutumu utawala vamizi wa Israel kwa "mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu."
Ikumbukwe kuwa, Novemba mwaka jana (2024) Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, ambako utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na kufanya mauaji ya kimbarii tangu mwezi wa Oktoba mwaka 2023.