Zawadi ya dola trilioni moja kwa Musk mkabala wa njaa inayowakabili Wamarekani milioni 42; Uadilifu au mkanganyiko?
-
Elon Musk
Huku mamilioni ya Wamarekani wakihangaika kumudu milo yao ya kila siku, wanahisa wa Kampuni ya Tesla wamepasisha kifurushi cha fidia ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha dola trilioni moja kwa Elon Musk. Tofauti na kukinzana huku kukubwa kati ya utajiri wa mtu mmoja na umaskini uliokithiri wa mamilioni ya watu kumefichua taswira halisi ya pengo la pato nchini Marekani.
Mwezi huu wa Novemba Marekani imeshuhudia moja ya vielelezo vya wazi zaidi vya kutokuwepo uadilifu wa kiuchumi. Wanahisa wa kampuni ya Tesla, kwa zaidi ya asilimia 75 ya kura, wamepasisha kifurushi kikubwa cha fidia ya dola trilioni moja kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Elon Musk. Kifurushi hicho, kilichotayarishwa kwa malengo kama vile kuongeza thamani ya soko la Tesla hadi dola trilioni 8.5 na kuuza mamilioni ya roboti za humanoid n.k, kingemsukuma Musk, ambaye utajiri wake sasa unakadiriwa kuwa dola bilioni 473, kuelekea kuwa trilionea wa kwanza duniani. Bila ya kuzingatia mshahara wake wa kila mwezi, Musk atapata hisa ya ziada ya dola trilioni moja ikiwa malengo haya yatafikiwa, na hivyo kuongeza umiliki wake kutoka asilimia 13 hadi 25.
Uamuzi huu uliohalalishwa na bodi ya Tesla kama wenzo wa kulinda "fikra" ya Musk, umechukuliwa huku mamilioni ya wananchi wa Marekani wakiwa katika mgogoro wa njaa. Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni, karibu watu milioni 47 ambao zaidi ya milioni 42 miongoni mwao wanaishi katika kaya zisizo na uslama wa chakula, wananataabika kwa ukosefu wa chakula cha kutosha.
Mgongano huu sio tukio la kihabari tu, bali pia ni kielelezo cha kuongezeka pengo la pato huko Marekani, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi duniani. Pengo la mapato nchini Marekani, ambalo limetambuliwa kuwa mojawapo ya changamoto za kimfumo za nchi hiyo kwa miongo kadhaa, limeongezeka kwa kasi zaidi katika miaka ya hivi karibuni. Gini Coefficient, kipimo cha kawaida cha ukosefu wa usawa wa mapato, mwaka huu kimefikia kiwango cha 0.42 nchini Marekani; takwimu inayodhihirisha namna mali nyingi zilivyorundikana mikononi mwa matajiri wachache wa nchi hiyo.
Data za Idara ya Takwimu ya Marekani na Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa mgao wa kipimo cha ukosefu wa usawa wa mapato mwaka 2023 ulikuwa karibu 0.41, na utabiri unaonyesha kuwa kiwango hicho kitaongezeka. Ongezeko hili linatokana na sera za uchumi ya Uliberali-Mamboleo: kupunguzwa tozo la ushuru kwa matajiri, kudhoofisha vyama vya wafanyakazi na kujikita kwenye uwekezaji wa teknolojia ambao huweka faida kwenye mifuko ya wasomi badala ya kuisambaza kwa njia ya uadilifu.
Katika hali ambayo kima cha chini cha mshahara nchini Marekani kimesalia kuwa kilekile tangu 2009, utajiri wa mabilionea kama Elon Musk umeongezeka kadri hisa za teknolojia zinavyopanda. Bonasi ya Tesla kwa Musk imezidisha pengo liliopo. Wakosoaji wakiwemo wanaharakati wanaotetea maslahi ya wafanyakazi wanaamini kuwa, bonasi hiyo ni "wizi wa kisheria." Hata kama Musk atafikia malengo machache tu ya awali, lakini ataweka mfukoni mamia ya mabilioni ya dola huku wafanyakazi wa Kampuni ya Tesla wenye wastani wa mishahara ya dola 20,000 hadi 30,000 kwa mwaka wakipambana na mfumuko wa bei wa asilimia 3 hadi 4 na kupanda kwa bei za vyakula.
Zawadi hiyo ya kitita cha fedha ambayo ni zaidi ya bajeti ya kila mwaka ya programu ya msaada wa chakula ya Marekani, imeandaliwa kulingana na malengo ya uendeshaji kama vile kuzalisha roboti milioni moja za Optimus. Hata hivyo hatari ya kusambaratika hisa za kampuni hiyo zinabebwa na jamii. Wakati huo huo kusambaratika kwa Kampuni ya Tesla kutapekekea kupotea maelfu ya ajira.
Mkabala wa mchezo huu, Wamarekani milioni 42 wanaendelea kutaabika kwa njaa. Idadi hiyo, ambayo inajumuisha watoto milioni 14, ni ya juu zaidi katika muongo mmoja wa karibuni. Sababu kuu za tatizo hili kubwa ni mfumuko wa bei wa chakula wa asilimia 20 tangu mwaka 2020, ukosefu wa ajira uliofichwa katika sekta za huduma na kupunguzwa kwa bajeti kwa programu kama vile SNAP (progarmu za misaada ya chakula).
Katika majimbo kama Arkansas, viwango vya uhaba wa chakula vinafikia asilimia 18.9, na katika jamii za Wamarekani weusi na walatino kiwango hicho ni zaidi ya asilimia 60. Njaa hii si tu inatishia afya lakini pia inaendeleza umaskini.
Wakati Musk anazungumzia "kumaliza umaskini duniani" na roboti zake, mamilioni ya Wamarekani wanategemea kuponi za chakula, na serikali ya Trump pia imepunguza bajeti ya misaada ya chakula. Mgongano na mkanganyiko huu unatoa mafunzo ya kina kuhusu mtindo wa kiuchumi wa Marekani.
Bonasi ya Musk iliyoidhinishwa na wanahisa inaonyesha upendeleo wa hali ya juu wa wanahisa" kuliko uadilifu wa kijamii. Lakini je, mtindo huu ni endelevu? Historia inaonyesha kuwa ukosefu wa usawa uliokithiri husababisha mapinduzi au mageuzi. Kwa mfano, vuguvugu la Occupy Wall Street mwaka 2011 lilikuwa dhidi ya "asilimia 1," na hii leo wimbi jipya limejitokeza kutokana na kuongezeka uungaji mkono kwa sera kama vile ushuru wa mali (iliyopendekezwa na Bernie Sanders).
Mwishowe tunaweza kusema kuwa, pengo la mapato linaloongezeka nchini Marekani, na kitita cha zawadi cha dola trilioni 1 alichopatiwa Elon Musk huku watu milioni 42 wakitaabika kwa njaa, ni wito wa mabadiliko. Wanasiasa wanapaswa kuzingatia usawa wa kodi, kuongeza mishahara na kuwekeza katika elimu na afya. Bila mageuzi haya, Marekani itakuwa nchi yenye migongano na mambo yanayokinzana.