Palestina: Hati zilizotolewa na Uturuki za kukamatwa viongozi wa Israel ni 'ushindi kwa haki'
Palestina imesifu na kupongeza hatua ya Uturuki ya kutoa hati za kukamatwa viongozi 37 wa utawala wa kizayuni wa Israel na kuielezea kuwa ni 'ushindi kwa haki' huku ikizitolea mwito nchi zingine kufuata mfano wa Ankara.
Hati hizo zilizotolewa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikiali ya Istanbul zinawalenga viongozi waandamizi wa Israel, akiwemo waziri mkuu Benjamin Netanyahu, waziri wa vita Israel Katz, waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben-Gvir, mkuu wa jeshi Eyal Zamir, na kamanda wa vikosi vya wanamaji vya Israel David Saar Salama.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imeeleza katika taarifa: "hatua hii ya kisheria iliyochukuliwa kwa ujasiri inaakisi ushindi kwa msingi wa haki na ni mfano halisi wa irada na dhamira ya mataifa huru na viongozi wanaokataa sera ya kinga ya kutoadhibiwa ambayo baadhi ya nchi zimeipatia Israel".
Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imesisitiza kwamba hatua hiyo "pia inathibitisha kuwa mamlaka ya utekelezaji wa sheria katika kupambana na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ni ya ulimwengu mzima".
Wizara hiyo ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema hatua zilizochukuliwa na Idara ya mahakama ya Uturuki zinaakisi "msimamo wa kiwango cha juu wa kisheria na maadili na zinatuma ujumbe wa wazi kwamba wale wanaofanya uhalifu dhidi ya watu wa Palestina hawatahepa uwajibikaji, bila kujali vyeo vyao".
Itakumbukwa kuwa mnamo Novemba 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC ilitoa hati ya kukamatwa Netanyahu na waziri wa zamani wa vita wa utawala wa kizayuni Yoav Gallant kwa kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Hadi sasa utawala ghasibu wa Israel umeshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 69,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na kuwajeruhi wengine zaidi ya 170,000 katika vita vya kinyama na mauaji ya kimbari uliyoanzisha huko Ghaza Oktoba 2023.../