Maandamano Paris kulaani mauaji ya halaiki Sudan, UAE yashutumiwa kwa kuunga mkono RSF
Mamia ya waandamanaji walikusanyika Jumamosi karibu na Mnara maarufu wa Eiffel mjini Paris kulaani mauaji ya halaiki yanayoendelea nchini Sudan, huku wakiishutumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuwafadhili na kuwapatia silaha waasi wa RSF wanaotekeleza mauaji ya raia.
Wabunge wawili wa Ufaransa, Gabrielle Cathala na Carlos Martens Bilango, waliongoza maandamano wakionesha mshikamano na wananchi wa Sudan.
Waandamanaji walitenga dakika moja ya kimya kuwakumbuka raia waliouawa katika mji wa El-Fashir, makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini, moja ya maeneo yaliyoathirika vibaya na vita vinavyoendelea.
Mabango yaliyobebwa yalikuwa na ujumbe mzito kama vile: “Watu wa Sudan wanahangaika usiku na mchana kuendelea kuishi” na “Nyamaza watu wakiwa wamelala, si wakati wanapokufa”, yakisisitiza wito wao kwa dunia kutambua hali ya hatari inayowakumba raia wa Sudan.
Waandamanaji walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili kusitisha mauaji ya raia na kuunga mkono juhudi za amani nchini Sudan.
Tangu Aprili 15, 2023, jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa katika vita vya ndani ambavyo juhudi nyingi za upatanisho za kikanda na kimataifa zimeshindwa kuvimaliza. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa na vyanzo vya ndani, takriban watu 20,000 wameuawa na zaidi ya milioni 15 wamekimbia makazi yao.
Mapema Jumamosi, shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) lilieleza wasiwasi wake kuhusu usalama wa maelfu ya raia waliokwama ndani ya mji wa El-Fasher baada ya RSF kuudhibiti.
UAE imekumbwa na shutuma kwa kuhusika katika usambazaji wa silaha na mamluki waliotumika katika operesheni ya kuuteka mji huo. Ingawa ushahidi umetolewa katika ripoti za Umoja wa Mataifa na vyanzo vingine, UAE imekanusha madai hayo.
Mnamo Jumatano, kinara wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kama Hemedti, alikiri kuwa “matendo ya ukiukaji” yalifanywa na vikosi vyake katika El-Fashir, akidai kuwa kamati za uchunguzi zimeundwa.