Russia yaimarisha maandalizi ya vita ya nyuklia kufuatia maagizo ya Rais Putin
Wizara ya mambo ya nje ya Russia imeanza kuchukua hatua za kutathmini uwezo wa taifa katika nyanja za nyuklia, kufuatia maagizo ya Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje, Sergei Lavrov.
Lavrov aliwaambia waandishi wa habari siku ya Jumamosi kwamba: “Maagizo ya Rais Vladimir Putin aliyotoa katika kikao cha Baraza la Usalama mnamo Novemba 5 yamekubaliwa na utekelezaji wake umeanza. Umma utapewa taarifa kuhusu matokeo.”
Katika kikao hicho, Putin aliagiza wizara za mambo ya nje na ulinzi, pamoja na vyombo maalum vya usalama na taasisi husika za kiraia, kuandaa mapendekezo kuhusu uwezekano wa Russia kufanya majaribio ya silaha za nyuklia.
Lavrov pia alieleza kuwa Moscow bado haijapata ufafanuzi kuhusu kauli za hivi karibuni za Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu kurejeshwa kwa majaribio ya silaha za nyuklia ya Washington.
Mnamo Oktoba 30, Trump alitoa agizo la kuanza mara moja majaribio ya silaha za nyuklia kwa misingi ya “usawa” na mataifa mengine yenye silaha za nyuklia, hatua iliyofuta rasmi marufuku ya majaribio hayo iliyokuwepo tangu mwaka 1992.
Trump alidai kuwa alichukia kutoa agizo hilo lakini “hakuwa na chaguo” kutokana na hofu yake binafsi ya mataifa mengine yenye silaha za nyuklia kuipiku Marekani.
Lavrov amesisitiza kuwa Russia inaendelea kufuatilia kwa karibu mwelekeo wa hali ya kimataifa, huku ikihakikisha kuwa taratibu zake za kiusalama zinabaki wazi na zinazingatia kikamilifu wajibu wa kimataifa.
Katika kikao hicho, Putin alionya kuwa Russia itachukua hatua za kujibu kwa usawa iwapo Marekani itarejesha majaribio ya silaha za nyuklia.
Wataalamu wa masuala ya kimataifa wameonya kuwa uamuzi wa Trump unaweza kudhoofisha juhudi za miongo kadhaa za kimataifa zilizolenga kuzuia kurudiwa kwa maafa ya kihistoria.
Aidha, wameeleza wasiwasi kuwa utawala wa Israel, mshirika wa karibu wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ambao ni mmiliki pekee wa silaha za nyuklia katika ukanda huu, unaweza kutumia uwezo wake wa silaha hizo haribifu kuendeleza jinai na kupora ardhi zaidi za nchi za eneo.