Kujiunga Wazungu na harakati ya kuisusia Israel; mabadiliko ya kweli au mashinikizo ya umma?
Harakati ya kususia bidhaa za Israeli (BDS) inazidi kupata nguvu kote duniani, tena kwa kasi kubwa, na watu binafsi na taasisi mbalimbali kote ulimwenguni zinajiunga nayo kwa lengo la kuongeza mashinikizo kwa Israel. Katika uamuzi muhimu zaidi wa hivi karibuni, ni nchi ya Ulaya ya Uholanzi kutangaza kwamba inaandaa sheria ya kupiga marufuku kuingiza nchini humo bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.
Kwa mujibu wa Pars Today, kuzidi kupata nguvu kampeni ya kususia bidhaa za Israel kunaendelea kutoa pigo kwa utawala wa Kizayuni huku nchi nyingi tofauti zikizidi kujiunga na harakati hiyo ya kiungwana. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, David van Weel amesisitiza kwamba nchi hiyo inaandaa sheria ya kupiga marufuku kuingiza bidhaa zinazozalishwa kwenye maeneo ya Wapalestina yaliyotekwa na Israel. Uamuzi huo umezidi kuongeza mashinikizo ya walimwengu dhidi ya Wazayuni kutokana na vitendo vyao vya kukiuka kupindukia haki za binadamu za Wapalestina.
Harakati ya Kususia bidhaa za Israel kwa kifupi BDS, iliyoanzishwa mwaka wa 2005 na zaidi ya asasi 170 za kiraia za Palestina, ilianzishwa kufuata mfano wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na lengo lake kuu ni kuilazimisha Israel kuheshimu sheria za kimataifa. Harakati hiyo imetoa mwito wa kukomeshwa uvamizi wa ardhi za Palestina na kurejea wakimbizi wa Palestina, na imechagua kususia bidhaa na huduma zinazotolewa na Israel kama moja ya njia za kuuwekea mashinikizo makubwa zaidi utawala wa Kizayuni.
Ingawa watu na taasisi nyingi zimejiunga na harakati hiyo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni lakini tangu yalipoongezeka mashambulizi dhidi ya Ghaza na kukiukwa kupindukia haki za Wapalestina, harakati hiyo imekuwa pana zaidi. Hivi sasa, serikali pia zimejiunga na harakati hiyo ya kimataifa. Uamuzi wa Uholanzi ni hatua muhimu katika kukabiliana na sera za kivamizi za utawala wa Kizayuni, hasa katika wakati huu ambapo Israel imefanya jinai za kuchupa mipaka kwa muda wa miaka miwili huko Ghaza.
Amma swali linalojitokeza hapa ni kwamba, ni mambo gani ambayo yamesababisha nchi za Ulaya kama Uholanzi kujiunga na harakati hiyo? Sababu muhimu zaidi ni mashinikizo ya wananchi. Wakati mamilioni ya watu wanapotuma ujumbe wa pamoja mitaani na kwenye mitandao ya kijamii, serikali haziwezi tena kupuuza nguvu hiyo ya wananchi. Wanasiasa hukumbwa na wasiwasi kuhusu athari za mashinikizo ya umma na ya wapiga kura wao, hivyo hulazimika kubadilisha sera zao. Hali inaonekana katika nchi zote za Ulaya, Amerika Kusini, Afrika na baadhi ya nchi za Asia.
Kwa mtazamo wa kisheria, kushirikiana na utawala vamizi ambao ni mkiukaji mkubwa wa haki za binadamu kuna gharama kubwa hivi sasa. Serikali za nchi mbalimbali zinalazimika kupasisha sera za kujiweka kwenye mazingira salama kwa kuhofia matokeo ya kisheria, kupungua uungaji mkono wa wananchi na kupoteza sifa na itibari zao kimataifa. Ndio maana kuendelea kushirikiana kibiashara na utawala vamizi wa Israel kumekuwa ni hatari kubwa kwa nchi za Magharibi hivi sasa.
Amma katika upande wa kiuchumi na kutokana na kupungua mauzo ya bidhaa zinazozalishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel na hasa baada ya kutokea maandamano makubwa ya wanunuzi wa bidhaa wanaosusia bidhaa za Israel, hivi sasa mashirika na serikali za nchi mbalimbali zinawawia vigumu kuendelea kushirikiana na utawala vamizi wa Kizayuni. Vikwazo na mashinikizo hayo, hasa wakati wa vita vya Ghaza, yamesababisha kupungua kwa 30% mauzo ya bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni. Wakati huo huo, uwekezaji wa kigeni katika maeneo ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni umepungua sana, kwani makampuni na wawekezaji hawataki kuhusisha majina yao na miradi kama hiyo ambayo inajulikana na walimwengu kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu.
Hii ni kusema kuwa, harakati za wanafunzi kote ulimwenguni, vyama vya wafanyakazi, wasanii na hata maduka ya rejareja yameweka mashinikizo ya moja kwa moja ya kiuchumi kwa mashirika tofauti ili yaondoe na yaache kabisa kuuza bidhaa zinazodhaniwa tu kuwa zimezalishwa Israel. Kampeni za kimataifa kwenye mitandao ya kijamii pia zimefanya sauti za mamilioni ya watu ziyafikie makampuni hayo na mashirika mengi yamelazimika kulegeza misimamo na mengine kulazimika kufanya ushirikiano wa siri na Israel, kutokana na mashinikizo ya walimwengu.
Kususia bidhaa zinazozalishwa katika maeneo ya Palestina yaliyotekwa na utawala wa Kizayuni kuanzia mwaka 1967 si pigo la kiuchumi tu kwa Israel; bali pia ni uthibitisho kwamba haki za wananchi wa Palestina si kitu cha kuchezewa tena na kwamba hakuna mtu anayeweza kuficha ukweli kupitia mabavu ya kijeshi na uwekezaji wa kiuchumi. Vikwazo dhidi ya Israel vina ujumbe wa wazi kwamba, haki za binadamu zinapokiukwa, hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha jambo hilo hata kwa mabavu ya kijeshi na kujiimarisha kiuchumi.
Kwa kweli, uamuzi wa Uholanzi wa kujiunga na harakati za kimataifa za kususia bidhaa za Israel si tu umetokana na mashinikizo la kijamii na misimamo thabiti ya walimwengu, lakini pia unaonesha kwamba hata nchi za Ulaya, ambazo huko nyuma zilikuwa ni wafuasi muhimu wa kisiasa na kiuchumi wa utawala vamizi wa Kizayuni, sasa hivi ziko chini ya mashinikizo ya wananchi wao ambao wameapa kuwa hawatokaa kimya tena mbele ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Uamuzi wa serikali ya Uholanzi wa kujiunga na kampeni ya kususia bidhaa za Israel ni sehemu ya wimbi kubwa zaidi la ususiaji; wimbi ambalo lilianzia katika ngazi ya watu wa kawaida na sasa limefikia hadi kuwa sera za serikali.
Kiujumla ni kwamba, uamuzi wa Uholanzi wa kujiunga na harakati za kususia bidhaa za Israel ni onyo kwa serikali na makampuni mengine kwamba kuunga mkono uvamizi na ukiukwaji wa wazi wa haki za binadamu, iwe ni kupitia njia za kiuchumi au kisiasa, ni mambo yasiyokubalika kabisa. Hatua hiyo ya kupongezwa na kupigiwa mfano ni hatua nyingine ya kuelekea kwenye ulimwengu ambao hauko tayari tena kukaa kimya mbele ya ukatili na jinai za kupindukia za Israel na hayo ni sehemu ya matunda ya Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa iliyoongozwa na HAMAS Oktoba 7, 2023.
Hapa chini tumeweka picha zaidi za ukatili wa Israel huko Ghaza: