Jarida la Wall Street: Makampuni ya Marekani yalipata mabilioni ya dola kutokana na vita dhidi ya Gaza
-
Wall Street Journal: Makampuni ya Marekani yanafaidika na vita vya Gaza
Jarida la Wall Street limefichua kwamba vita vya miaka miwili vya Ukanda wa Gaza havikuwa tu janga kubwa la binadamu, bali pia muamala mkubwa wa biashara kwa makampuni ya Marekani yaliyopata mabilioni ya dola kutokana na mauzo ya silaha kwa Israel, kwa msaada mpana wa kisiasa na kiuchumi kutoka Washington.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benoît Faucon, uchambuzi wa gazeti hilo kuhusu data ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani umeonyesha kuwa Washington iliidhinisha mauzo ya silaha yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 32 kwa Israel tangu Oktoba 2023, ikiwakilisha ongezeko kubwa la misaada ya kawaida ya kijeshi.
Jarida hilo limeongeza kuwa, mauzo haya "yalijenga safu isiyo na kifani ya usambazaji wa silaha za Marekani kwa Israel, na kuunda mtiririko endelevu wa faida, ambao wanufaika wake wakuu walikuwa makampuni kama vile Boeing, Northrop Grumman, Lockheed Martin, General Dynamics na Caterpillar."
Boeing ndiyo iliyopata faida kubwa zaidi, baada ya kupata idhini ya mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 26, ikiwa ni pamoja na mauazo ya ndege za kivita za F-35 na mabomu yanayoongozwa. Makampuni mengine pia yamefaidika na mikataba ya kuiuzia Israel makombora ya vifaru, vipuri na magari ya kivita.
Jarida hilo limesema kwamba mzigo wa kifedha wa mikataba hiyo ulibebwa na walipa kodi wa Marekani, baada ya ufadhili wa kijeshi wa Marekani kwa Israel kupanda kutoka dola bilioni 3.3 kila mwaka hadi dola bilioni 6.8 mwaka jana, bila kuhesabu misaada isiyo ya moja kwa moja.
Licha ya ukosoaji wa kimataifa na maafa ya binadamu yaliyosababishwa na vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza vilivyoua zaidi ya Wapalestina 68,000, mikataba ya kijeshi inaendelea kutiririka, ikichochewa na masuala ya kiusalama na kimkakati ya Marekani, na kwa maslahi ya makampuni yanayotaka kudumisha uzalishaji na kupanua faida zao.