Mamdani: Ikiwa Netanyahu atakuja New York katika mkutano ujao wa UNGA nitaamuru akamatwe
Meya Mteule wa jiji la New York Zohran Kwame Mamdani ameambia televisheni ya ABC News kwamba atatoa hati ya kukamatwa waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu endapo ataingia ndani ya ardhi ya Marekani mwaka ujao kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mamdani amesisitiza kwamba atafanya kila awezalo kuandaa njia za kisheria za kutekeleza hati za kimataifa za kukamatwa Netanyahu.
Meya huyo mteule wa New York amefafanua kwa kusema: "nimeshaeleza mara kadhaa kwamba jiji hili linafuata sheria za kimataifa, na sheria hizi zitatekelezwa wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika katika jiji hili mwaka ujao. Miongoni mwa hati ambazo lazima zitekelezwe ni hati za ukamataji za Mahakama Kuu ya The Hague."
Mamdani ameendelea kubainisha: "haijalishi kama hati hizo zimetolewa dhidi ya Benjamin Netanyahu au Vladimir Putin; sisi tunafungamana na maadili yetu".
Katika mahojiano hayo na ABC News, meya huyo mteule wa New York ameeleza pia: "tofauti na Donald Trump, mimi ninafanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria na sio mimi kuweka sheria. Kwa hivyo, nitafanya niwezavyo kutekeleza hati za kimataifa."
Meya huyo mpya wa New York amesisitiza kwa kusema: "ikiwa Netanyahu atakuja New York na ikawa mimi sijafanya jitihada za kumkamata, sitokuwa Meya wa New York".
Mamdani ameongezea kwa kusema: "lazima tutumie uwezo wote wa kisheria kutekeleza hati ya kukamatwa Netanyahu".../