Mashtaka ya ICC dhidi ya Trump: Jinamizi kwa Ikulu ya White House?
Ikulu ya Rais wa Marekani, White House, ina wasiwasi kuhusu uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutoa kibali cha mashtaka dhidi ya Donald Trump.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba Ikulu ya White House inashauriana na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ili kuzuia kufunguliwa mashtaka dhidi ya Rais wa Marekani. White House ina wasiwasi hasa kuhusu kufunguliwa mashtaka dhidi ya Donald Trump baada ya muhula wake wa urais kumalizika mwaka wa 2029, na kwa hivyo inataka kubadilishwa Mkataba wa Roma ili kutoa kinga kwa maafisa wa serikali ya Marekani. Washington imeonya kwamba itaweka vikwazo vipya kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iwapo haitakubali kutupilia mbali nia ya kufungua kesi dhidi ya Trump au maafisa wakuu katika serikali yake. Mashambulizi dhidi ya Iran, Somalia, Yemen, Karibia na msaada wa silaha kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni miongoni mwa masuala ambayo yanaweza kuwa sababu ya kumfungulia mashtaka Doland Trump kwa tuhuma za kutenda uhalifu wa kivita.
Katika suala hili, serikali ya Marekani imewasiliana kwa siri na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kutishia kuweka vikwazo vipya dhidi ya taasisi hiyo ya kimataifa iwapo mahakama hiyo itajaribu kumfungulia mashtaka Rais wa Marekani Donald Trump. Washington imewafahamisha wanachama wa mahakama hiyo, wakiwemo baadhi ya washirika wa Marekani, kuhusu suala hili. Marekani si mwanachama wa Mkataba wa Roma, na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai inaweza tu kuwafungulia mashtaka wakuu wa nchi katika hali ya dharura.
Hapo awali, utawala wa Trump uliwawekea vikwazo baadhi ya maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kutoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita, Yoav Gallant, ambao wanatuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita na mauaji ya kimbari huko Gaza. Mapema Juni 2025, Marekani ilitangaza kwamba imewawekea vikwazo majaji wanne wa mahakama ya ICC kwa kushiriki katika hatua za kuchunguza uhalifu wa Israel na kutoa hati za kukamatwa viongozi wa utawala huo kwa kuhusika kwao na mauaji ya kimbari.
Rais wa Marekani, Donald Trump pia amechukua msimamo mpya, akiitishia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na kuitaka taasisi hiyo isimamishe uchunguzi wake dhidi ya utawala wa Israel na Marekani. Trump ametishia kwamba hataruhusu wanajeshi wa Israel au Marekani waliopigana kwenye mstari wa mbele kushtakiwa mahakamani.
Ikulu ya White House imetangaza kwamba kama ICC haitakidhi matakwa ya Trump, itakabiliwa na vikwazo vikali ambavyo vitaharibu pakubwa uwezo wa mahakama na majaji wake kuendelea na kazi yao. Haya yanajiri huku Ikulu ya White House ikiwa na wasiwasi kuhusu kutolewa kibali cha kumshtaki Trump kwa kutenda uhalifu wa kivita.
Inaonekana kwamba uwezekano wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutoa hati ya kukamatwa Donald Trump ni jinamizi baya la kisiasa na kisheria kwa Ikulu ya White House; kwani suala hilo linaweza kuwa na matokeo mabaya kwa nafasi ya Marekani katika mfumo wa kimataifa, uhusiano wa kidiplomasia na hata uhalali wa ndani wa nchi hiyo.
Kwanza kabisa, ikumbukwe kwamba Marekani si mwanachama wa Mkataba wa Roma, hati iliyoanzisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Hii ina maana kwamba Washington haitambui mamlaka ya mahakama hiyo na imekuwa ikijaribu kuwalinda raia na maafisa wake wasifunguliwe mashtaka ya kimataifa. Hata hivyo, ICC inaweza kuchukua hatua dhidi ya wakuu wa nchi katika mazingira makhsusi, hasa kunapotolewa mashtaka ya uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari au uhalifu dhidi ya binadamu. Katika kesi ya Trump, baadhi ya vitendo vyake vya kijeshi na kisiasa katika maeneo mbalimbali ya dunia, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kushambulia Iran, mashambulizi ya Marekani dhidi ya Somalia na Yemen, na misaada ya silaha kwa Israel katika mauaji ya kimbari ya watu wa Gaza, vinaweza kutayarisha msingi wa kuwasilisha malalamiko na mashtaka ya kisheria.
Kisiasa, uamuzi wa kufunguliwa mashtaka dhidi ya Trump unaweza kuwa pigo kubwa kwa hadhi na nafasi ya Marekani. Washington imekuwa ikijionyesha kama mtetezi wa haki za binadamu na mfumo wa kimataifa, lakini iwapo kutatolewa kibali cha kimataifa cha kukamatwa Rais wa Marekani, hatua hiyo itachafua sana sura hiyo bandia na ya uongo. Katika hali kama hiyo, washirika wa Marekani pia watakabiliwa na hali ngumu: Ama kudumisha uhusiano wa kimkakati na Washington au kutimiza wajibu wao wa kisheria na kimaadili kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Hali hiyo inaweza kusababisha nyufa katika miungano ya kijadi ya Marekani na kupunguza imani ya kimataifa kwa uongozi wa nchi hiyo.
Kwa mtazamo wa kisheria, wasiwasi wa Ikulu ya White House unatokana na ukweli kwamba, kutolewa hati ya kukamatwa dhidi ya Donald Trump kunaweza kuweka rekodi na mfano hatari. Kwani, kama Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inaweza kumfungulia mashtaka Rais wa Marekani, inawezekana kwamba maafisa wengine wa Marekani pia watakabiliwa na tishio kama hilo katika siku zijazo. Kwa sababu hiyo, serikali ya Marekani imewasiliana na ICC na hata kutishia kuweka vikwazo zaidi dhidi ya taasisi hiyo ya kimataifa. Msimamo kama huo unaonyesha kwamba Washington ina wasiwasi wa kupoteza kinga ya kijadi ya kushtakiwa maafisa wake kimataifa kuliko kitu kingine chochote.
Kwa mtazamo wa ndani, jambo hilo linaweza pia kuwa na matokeo mabaya. Trump si rais wa sasa tu bali pia ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za ndani za Marekani. Hivyo, kutolewa hati ya kukamatwa kwake kunaweza kuzidisha mvutano wa kisiasa ndani ya nchi, kuchochea zaidi makabiliano baina ya wapinzani na wafuasi wake, na hata kuhoji uhalali wa taasisi za kisiasa za Marekani.
Hatimaye, jinamizi la Ikulu ya White House linaeleweka vyema kutokana na mtazamo kwamba, kutolewa kibali cha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai cha kukamatwa Donald Trump hakutakuwa mgogoro wa kisheria pekee, bali pia mgogoro kamili wa kisiasa na kidiplomasia. Uamuzi huo unaweza kuiweka Marekani katika hali inayoilazimisha kuchagua kati ya kumtetea rais wake au kudumisha uhusiano wa kimataifa. Hali kama hiyo ni ngumu sana na yenye gharama kubwa kwa nchi inayojiona kuwa yenye nguvu na kiranja wa dunia.