Putin atangaza kumuunga mkono Maduro licha ya US kushadidisha vitisho dhidi ya Venezuela
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema, anamuunga mkono Rais wa Venezuela Nicolas Maduro wakati huu ambapo Marekani imejizatiti kijeshi katika eneo la Carribean huku ikishadidisha vitisho dhidi ya Venezuela.
Viongozi hao wametilia mkazo uhusiano wa karibu uliopo kati ya Moscow na Caracas katika mazungumzo waliyofanya kwa njia ya simu jana Alkhamisi.
Kwa mujibu wa Ikulu ya Russia, Kremlin, Putin "ametangaza mshikamano na watu wa Venezuela na kusisitizia tena uungaji mkono wake kwa uamuzi wa serikali ya Maduro wa kutetea maslahi ya taifa na uhuru dhidi ya mashinikizo ya kigeni".
Aidha, marais wa Russia na Venezuela wamethibitisha tena msimamo wao wa kufungamana na mkataba wa ushirikiano wa kimkakati uliosainiwa na nchi zao mnamo mwezi Mei mwaka huu.
Serikali ya Venezuela imesema, katika mazungumzo hayo ya simu, Putin na Maduro vilevile wametilia mkazo kuhusu "hali ya kimkakati, imara, na inayokua ya mahusiano baina ya pande mbili."
Aidha, Caracas imeongeza kuwa kiongozi wa Russia ameunga mkono juhudi zinazofanywa na Maduro za "kuimarisha amani, utulivu wa kisiasa, na maendeleo ya kiuchumi" nchini Venezuela.
Mazungumzo hayo yamefanyika baada ya Marekani kuikamata meli ya mafuta iliyoondoka bandarini Venezuela mapema mwezi huu.
Venezuela imeielezea operesheni hiyo kuwa ni kitendo cha uharamia na kuishutumu Marekani kwa kutaka "kupora" maliasili zake.../