Trump, Clinton na Gates waonekana katika seti mpya ya picha za Epstein
-
Trump aonekana katika picha mpya za Epstein
Wanachama wa chama cha Democratic katika Congress ya Marekani wamefichua picha mpya zinazomdhihirisha Rais wa Marekani, Donald Trump, Rais wa zamani Bill Clinton, mwanzilishi wa Microsoft Bill Gates na watu wengine wenye ushawishi wakiwa pamoja na mfanyabiashara aliyepatikana na hatia ya kufanya biashara haramu ya ngono ya watoto, Jeffrey Epstein.
Trump anaonekana katika picha 3 kati ya 19 zilizotolewa na wanachama wa chama cha Democratic wa Kamati ya Usimamizi ya Congress, ambao wanasema wanapitia zaidi ya picha 95,000 zilizotolewa na wasimamizi wa mali ya Epstein.
Wengine wanaoonekana kwenye picha zilizochukuliwa kutoka kwenye mali ya Epstein, aliyetuhumiwa kufanya magendo ya watoto wadogo waliotumiwa katika utumwa wa ngono, ni pamoja na Mwanamfalme wa zamani wa Uingereza, Andrew, ambaye sasa anajulikana kama Andrew Mountbatten-Windsor, mkurugenzi wa filamu Woody Allen, mfanyabiashara Richard Branson, na mpangaji mikakati ya kisiasa wa mrengo wa kulia, Steve Bannon, ambaye ni mshirika wa Donald Trump.
Trump anaonekana katika picha kadhaa, ikiwemo moja ambapo amesimama karibu na Epstein, na nyingine ambapo amezungukwa na wanawake sita waliovaa taji za maua.
Mwakilishi wa chama cha Democratic, Robert Garcia, wa kamati ya usimamizi ya Congress, amesema kwamba "picha hizo za kukera zinaibua maswali zaidi kuhusu Epstein na uhusiano wake na baadhi ya watu wenye nguvu zaidi duniani."
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, nyaraka zinazohusiana na Jeffrey Epstein, bepari na bilionea aliyepatikana na hatia ya biashara ya ngono ya watoto, zimeanika peupe uhusiano wa siri aliokuwa nao na watu mashuhuri na vilevile shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad.
Mlanguzi huyo wa ngono pia alikuwa na mawasiliano na baadhi ya watu mashuhuri wa Marekani, wakiwemo Kevin Spacey na Chris Tucker, na pia amemshauri Elon Musk kuhusu mambo tofauti.
Epstein aliunda mduara wa watu mashuhuri na kuwawezesha kutumia kingono idadi kubwa ya wanawake na watoto, ambapo alishirikiana na wasaidizi wake kuwanyanyasa kingono.
Jeffrey Epstein anadaiwa kujiua gerezani mnamo 2019 akisubiri kusikilizwa kesi yake ya mashtaka ya biashara ya ngono. Hata hivyo mawakili wa Epstein wanapinga matokeo ya uchunguzi wa sababu ya kifo chake wakisema kuwa kuna shaka kubwa kuhusu chanzo halisi cha kifo hicho, na hivyo kuchochea dhana kuwa aliuawa.