Waziri Mkuu wa Uhispania: Kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i134306-waziri_mkuu_wa_uhispania_kampeni_ya_marekani_katika_maji_ya_karibi_ni_ukiukaji_wa_sheria_za_kimataifa
Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kwamba kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.
(last modified 2025-12-14T22:48:21+00:00 )
Dec 14, 2025 22:48 UTC
  • Waziri Mkuu wa Uhispania: Kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa
    Waziri Mkuu wa Uhispania: Kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa

Waziri Mkuu wa Uhispania amesema kwamba kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Pedro Sanchez amekosoa kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi inayofanyika kwa kisingizio cha kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, akiitaja kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa na ametoa wito wa kupatikana suluhisho la amani ya mzozo huo.

Sanchez amesema kampeni ya Marekani katika maji ya kimataifa ambayo Marekani inadai inalenga kupambana na eti biashara haramu ya dawa za kulevya katika Bahari ya Karibi ni changamoto kwa sheria za kimataifa na inaibua maswali mengi iwapo kweli Magharibi inaheshimu kanuni zake.

Katika mahojiano ya kipekee na jarida la Italia "Les Presso" toleo la Ijumaa Disemba 12, Waziri Mkuu wa Uhispania alisema: "Marekani inafanya mauaji katika maji ya kimataifa bila utaratibu wa mahakama na kwa kisingizio cha kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya." Amesema changamoto kama hiyo kwa sheria za kimataifa "inatia wasiwasi sana" na kuongeza: "Kampeni ya Washington inaimarisha mtazamo kwamba Magharibi ina mienendo inayokinzana katika kutekeleza kanuni zake."

Pedro Sanchez

Katika miezi ya hivi karibuni utawala wa Trump umeanzisha operesheni ya kijeshi katika Bahari ya Karibi kwa kisingizio cha kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, na imepeleka huko vikosi na zana kubwa za kijeshi. Ripoti zinasema kuwa, operesheni hiyo hadi sasa imesababisha uharibifu wa meli nyingi na mauaji ya zaidi ya watu 83 katika mashambulizi ya jeshi la Marekani.

Msimamo huo wa Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, kama nchi ambayo ni mwanachama muhimu wa Umoja wa Ulaya na NATO, kuhusu vitendo haramu vya Marekani katika Bahari ya Karibi na tishio la kushambulia Venezuela unatambuliwa kuwa na umuhimu mkubwa. Anasema, kampeni ya Marekani katika maji ya Karibi inakiuka sheria za kimataifa kutokana na hatua za kijeshi zinazochukuliwa bila utaratibu wa mahakama na ni tishio kwa usalama na amani ya kikanda na kimataifa.

Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, uwepo kijeshi wa nchi fulani katika maji huru ya kimataifa unaruhusiwa tu ikiwa umeidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au unafanyika ndani ya mfumo wa kujilinda. Kitendo cha Marekani cha kulipua meli na boti hizo, na vilevile amri ya "hakuna manusura anayepaswa kubakishwa hai" iliyotolewa na Waziri wa Vita wa Marekani, Pete Hegseth, vinatambuliwa kuwa ni kielelezo cha uhalifu wa kivita. Waziri Mkuu wa Uhispania anaamini kwamba mbinu kama hiyo, badala ya kuimarisha nidhamu ya kimataifa, itaivuruga na kusababisha hali ya kutoaminiana kati ya nchi mbalimbali. Ameonya kwamba mbinu kama hiyo itadhoofisha imani ya kimataifa kuhusu kufungamana nchi za Magharibi na maadili ya kisheria na kutoa picha inayokinzana juu ya madai ya Magharibi ya kutetea haki za binadamu.

Hata ndani ya Marekani kwenyewe, kuna upinzani dhidi ya operesheni hiyo. Baadhi ya makamanda wa jeshi wametilia shaka uhalali wa maagizo yaliyotolewa, jambo ambalo limepelekea kufukuzwa kazi mmoja wa makamanda wakuu wa jeshi la Marekani, Jenerali Alvin Holsey, aliyekuwa mkuu wa Kamandi ya Kusini (SOUTHCOM). Hitilafu hizi zinaonyesha kwamba, hata ndani ya jeshi la Marekani kwenyewe hakuna mwafaka  kuhusu uhalali wa vitendo hivyo. Zaidi ya hayo, baadhi ya wajumbe wa Kongresi wameeleza kutoridhishwa na mkakati wa serikali ya Trump katika eneo hilo na wametoa wito wa kuwepo uwazi zaidi.

Maduro na Trump

Operesheni ya kijeshi ya Marekani katika Bahari ya Karibi, ambayo inafanyika  huku kukiwapo mvutano unaoongezeka kati ya Washington na Caracas, pia ina mwelekeo muhimu wa kisiasa. Utawala wa Trump umeongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo ili kuweka mashinikizo zaidi kwa Venezuela, ambayo Marekani inadai inanufaika na biashara ya dawa za kulevya, na inatumia madai hayo kuhalalisha mashambulizi yake. Lakini wakosoaji, ikiwa ni pamoja na Uhispania, wanaviona vitendo hivyo kuwa ni jaribio la kuipindua serikali ya Maduro kwa kutumia mabavu. Pedro Sanchez anasisitiza kwamba sera kama hiyo haitatatua mgogoro wa Venezuela, bali pia itahatarisha amani ya eneo lote la Karibi. Waziri Mkuu wa Uhispania ametoa wito wa matumizi ya zana za kidiplomasia na mazungumzo ili kutatua mizozo huo, akionya kwamba kuendeleza mchakato huu kunaweza kusababisha mizozo mipana zaidi.

Msimamo huo wa Waziri Mkuu wa Uhispania ni mwangwi wa wasiwasi mpana wa Ulaya kuhusu sera na mienendo ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya Marekani katika uga wa kimataifa. Nchi nyingi za Ulaya zinaamini kwamba sera hiyo ya Washington ya kujichukulia maamuzi ya upande mmoja ya kijeshi siyo tu kwamba haisaidii kutatua matatizo ya kimataifa, bali pia yanatayarisha uwanja wa kujitokeza migogoro mipya.

Sanchez amesisitiza haja ya kurejea kwenye sheria za kibinadamu, akisema kwamba kuwaua watu katika maji ya kimataifa bila utaratibu wa mahakama ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu.