Gazeti la New York Times laorodhesha "uongo" wa Rais Trump katika mwaka mzima
-
Donald Trump
Gazeti la New York Times linaamini kwamba katika mwaka wa kwanza wa muhula wake wa pili, Rais wa Marekani Donald Trump amesema uongo mwingi, kutoa madai yasiyo na msingi na upotoshaji ili kuhalalisha mabadiliko na kudanganya kuhusu mafanikio katika maeneo ya uchumi, uhamiaji na kadhalika.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, hoja ya Rais Donald Trump ya kufanya mabadiliko makubwa nchini inatokana na utiaji chumvi usio sahihi, kama vile madai yake kwamba "mfumko mbaya zaidi wa bei" ulitokea chini katika utawala wa mtangulizi wake, Joe Biden, na kwamba kwa sasa Marekani ina takwimu "bora zaidi" chini ya utawala wake.
Gazeti la New York Times limechunguza sampuli za baadhi ya uongo uliotawala hotuba za Donald Trump katika mwaka wa kwanza wa muhula wake wa pili, ikiwa ni pamoja na kuhusu takwimu zilizotiwa chumvu kuhusu uhamiaji, uchumi, uwekezaji na mapambano dhidi ya mihadarati.
Kuhusu madai ya kuboreka uchumi katika kipindi chake, gazeti la New York Times linasema kwamba madai hayo si sahihi kwa sababu viashiria vingi havithibitishi kwamba uchumi umebadilika sana kutoka kuwa "mbaya" hadi "bora".
Gazeti hilo pia limekadhibisha madai ya uongo ya Trump kuhusu uwekezaji wa kigeni nchini Marekani ambao amesema umefikia dola trilioni 18 na kuandika kuwa, makadirio ya White House yanakadhibisha madai hayo yakisema kuwa uwekezaji ulikuwa nusu ya takwimu zilizotolewa na Trump.
New York Times pia limeanika uongo wa Rais wa Marekani kuhusu kuangamiza utoroshaji wa mihadarati kuingia nchini humo na kusema, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba mashambulizi ya kijeshi yaliyoidhinishwa na Rais Trump dhidi ya boti zinazotoka Venezuela yamefanikiwa kukomesha ulanguzi wa dawa za kulevya baharini.