"Haiwezi Tena Kuvumilika", asema Waziri Mkuu wa Ubelgiji akiitaka Ulaya iamue moja kuhusu Trump
https://parstoday.ir/sw/news/world-i135740-haiwezi_tena_kuvumilika_asema_waziri_mkuu_wa_ubelgiji_akiitaka_ulaya_iamue_moja_kuhusu_trump
Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever amesema, ni lazima Ulaya imueleze wazi Rais wa Marekani Donald Trump kwamba hali ilipofikia hivi sasa "Haiwezi Tena Kuvumilika".
(last modified 2026-01-21T10:39:27+00:00 )
Jan 21, 2026 10:39 UTC

Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever amesema, ni lazima Ulaya imueleze wazi Rais wa Marekani Donald Trump kwamba hali ilipofikia hivi sasa "Haiwezi Tena Kuvumilika".

"Kadiri unavyozidi kumridhia, ndivyo anavyozidi kushupaa," ameeleza De Wever kando ya Jukwaa la Uchumi Duniani linalofanyika mjini Davos, Uswisi.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji amesema, kurejesha uwezo wa kiushindani wa Ulaya lazima kiwe kipaumbele kisicho na shaka, lakini amesisitiza kwamba matamshi aliyotoa hivi karibuni Trump kuhusu Greenland na vitisho vya ushuru yametoa changamoto zaidi kwa Umoja wa Ulaya.

De Wever alitarajiwa kukutana na Trump leo Jumatano akiwa pamoja na Mfalme Philippe wa Ubelgiji na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte, ingawa ametilia shaka kama mkutano huo untafanyika.

Waziri Mkuu wa Ubelgiji amebainisha kuwa Ulaya lazima itoe mjibizo kwa kuimarisha soko lake la pamoja, kuongeza ushindani, na kuunda miungano mipya.

"Tunapaswa kujiimarisha wenyewe kijeshi," ameeleza De Wever na kuongezea kwa kusema: "Baraza la Ulaya lazima liongoze ajenda na kusema: fanya hivi, na si vinginevyo."

Katika mahojiano mengine tofauti aliyofanyiwa na mtangazaji wa Ubelgiji VRT NWS, De Wever amesema Ulaya lazima ibainishe wazi kuwa haitavumilia vitisho vya hatua za kijeshi dhidi ya eneo la mshirika wake.

"Tukiwa kama Ulaya, lazima tumwambie Trump: 'Hili linavyokwenda lisivuke zaidi ya hapa. Rudi nyuma au tukakwenda pamoja hadi mwisho'" ameeleza Waziri Mkuu wa Ubelgiji.

Ameongezea kwa kusema, ni dhahiri hivi sasa kwamba, Ulaya lazima ichukue hatua haraka na kwa kujiamini.../