Katibu Mkuu wa NATO: Ulaya 'iendelee kuota' kama inadhani inaweza kujilinda bila ya US
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte amesema, Umoja wa Ulaya, EU bali hata Ulaya nzima haina uwezo wa kujilinda bila ya Marekani na kusisitiza kuwa, nchi wanachama zitalazimika kutumia hadi 10% ya Pato lao la Taifa kwa ajili ya shirika hilo la kijeshi, ambayo inaweza pia isitoshe.
Rutte ameyasema hayo alipohutubia Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Usalama na Ulinzi ya Bunge la Ulaya mjini Brussels jana Jumatatu.
Katibu Mkuu wa NATO ametoa kauli hiyo huku baadhi ya maafisa wa EU wakiendelea kutoa wito wa kutaka kambi hiyo ya kijeshi iache kuwa na utegemezi mkubwa kwa Marekani katika masuala ya usalama. Katikati ya Januari, Kamishna wa Ulinzi Andrius Kubilius alidai EU inahitaji jeshi la kudumu la watu 100,000 ili iweze kujichukulia hatua na maamuzi yake kwa uhuru.
Kwa mujibu wa Rutte, mipango kama hiyo haiendani na uhalisia wa mambo, na akasisitiza katika hotuba yake: "ikiwa mtu yeyote hapa anafikiria tena, kwamba Umoja wa Ulaya au Ulaya kwa ujumla inaweza kujilinda bila Marekani, basi endelea kuota. Huwezi".
"Ikiwa unataka kweli kufanya hivyo peke yako, na wale unaowaomba kwa ajili ya hilo, sahau hilo, huwezi kamwe kufikia huko na 5%, itakuwa 10%" ameongezea kusema Katika Mkuu huyo wa NATO.
Rutte ameendelea kueleza katika hotuba yake: "lazima muimarishe uwezo wenu wa nyuklia unaogharimu mabilioni kwa mabilioni ya yuro. Mutapoteza, na hatimaye katika sinario hiyo, mutapoteza mdhamini mkuu wa uhuru wetu, ambao ni mwavuli wa nyuklia wa Marekani. Kwa hivyo, jamani, nakutakieni kila la kheri".
Hayo yanajiri katika hali ambayo, katika miezi ya karibuni, Umoja wa Ulaya umejihisi kuwa umetengwa na mshirika wake Marekani katika mazungumzo ya amani ya Ukraine yanayosimamiwa na Washington na wakati huohuo imekwaruzana na Marekani kuhusiana na njama ya rais wa nchi hiyo Donald Trump ya kutaka kuihodhi Greenland, hatua ambayo baadhi ya wanasiasa wa Ulaya wanasema inaweza kuhitimisha "enzi ya miaka 80 ya Uatlantiki" kwa maana ya ushirikiano wa Marekani na Ulaya.../