Guterres ataja vipaumbele vyake katika mwaka wake wa mwisho kama Katibu Mkuu wa UN
Katika wakati ambapo mivutano ya kimataifa inaongezeka huku hatua zisizo na tahadhari zikisababisha madhara hatari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa kuimarishwa juhudi za amani, haki na maendeleo endelevu.
Guterres alitoa wito huo jana Alkhamisi alipokuwa akiainisha vipaumbele vyake vya mwaka wa mwisho madarakani kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akisisitizia kuchaguliwa amani badala ya machafuko.
“Mwaka 2026 tayari unaonekana kuwa mwaka wa machafuko na mshangao wa mara kwa mara,” ameeleza Katibu Mkuu wa UN alipozungumza na waandishi wa habari jijini New York kwenye makao makuu ya umoja huo.
Guterres ambaye kitaaluma alisomea fizikia kabla ya kuingia kwenye maisha ya utumishi wa umma amesema, katika nyakati za mabadiliko makubwa, hurejea kwenye kanuni thabiti zinazoeleza jinsi nguvu zinavyofanya kazi.
Miongoni mwa kanuni hizo ni Sheria ya Tatu ya Mwendo ya Newton, inayosema kwamba kwa kila tendo kuna majibu sawa na ya kinyume.
Amesema “tunapoanza mwaka huu, tumeazimia kuchagua hatua zitakazochochea hatua halisi na chanya”.
Katibu Mkuu wa UN amezitaja hatua hizo kuwa ni “hatua za amani, za haki, za uwajibikaji, na za maendeleo katika nyakati zetu zenye misukosuko.”
Kwa mujibu wa Guterres, leo hii kutowajibika kunachochea migogoro na kuchangia kuongezeka mapigano, kupanua wigo wa kutoaminiana, na kuruhusu waharibifu wenye nguvu kuingilia kutoka pande zote.
“Wakati huohuo, kupunguzwa kwa msaada wa kibinadamu kunazalisha mnyororo wake wa athari mbaya za kukata tamaa, ufurushwaji wa watu na vifo, huku ukosefu wa usawa ukiendelea kuongezeka”, ameeleza Katibu Mkuu huyo wa UN anayekaribia kumaliza muda wake.
Aidha, amesema: “tunasisitiza amani ya haki na endelevu inayojengwa juu ya sheria za kimataifa. Amani inayoshughulikia chanzo cha migogoro. Amani inayodumu, zaidi ya kutiwa saini kwa makubaliano”.../