Afisa wa zamani wa Marekani: Washington imeshindwa kutimiza malengo yake dhidi ya Iran
-
Scott Ritter
Afisa wa zamani wa shirika la ujasusi la jeshi la majini la Marekani amesema Washington imeshindwa kutimiza malengo ya uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Scott Ritter ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kijeshi na mkaguzi wa zamani wa silaha wa Umoja wa Mataifa amesema, kinyume na ilivyokuwa ikidhaniwa, mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran yamekuwa na matokeo kinyume na matarajio.
Akizungumza kwa lugha ya kejeli, mkaguzi huyo wa zamani wa silaha wa Umoja wa Mataifa amesema, lengo la Marekani la kumuua Kiongozi Mkuu wa Iran lilikuwa kuwaburuta wananchi mitaani dhidi ya utawala, na leo mamilioni ya Wairani wameingia mitaani lakini kwa ajili ya kuomboleza mauaji ya kiongozi wao. Amesema: “Mfumo unaotawala nchini Iran unaungwa mkono sana na wananchi.”
Scott Ritter amesema uungaji mkono huo wa wananchi unazidi kuongeza kadiri mashambulizi ya Marekani na Israel yanavyozidi. Ameongeza kuwa Wairani wamejiandaa kwa vita hivi kwa zaidi ya miaka 20 yaani katika zama za vitisho vya Dick Cheney, na maandalizi hayo yamekamilika.
Afisa huyo wa zamani wa upelelezi wa Marekani amesema, Wairani wanaendelea kushambulia kambi na ngome za Marekani Mashariki ya Kati na wanaiadhibu vikali Israel kiasi ambacho Waisraeli hawakukifikiria akilini mwao.