Planet Labs inachuja picha za satalaiti za hasara za kambi za Marekani zinazotwangwa na Iran
-
Moja ya kambi ya Marekani iliyotwangwa na Iran
Kampuni ya huduma za satalaiti ya Marekani imetangaza kuwa, inachelewesha kutoa picha zake kwa siku nne ili kuzuia tathmini na uchambuzi wa hasara zilizosababishwa kwenye kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.
Kampuni ya huduma za picha za satalaiti ya Planet Labs imetangaza kuwa usambazaji wa picha mpya za Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na picha kutoka nchi za Ghuba ya Uajemi na Iraq na Kuwait unacheleweshwa kwa masaa 96 ili kuzuia uchambuzi wa hasara za kambi za Marakani katika eneo hilo.
Planet Labs imewajulisha wateja wake kwamba tangu sasa baadhi ya picha za satalaiti za Asia Magharibi zitacheleweshwa kwa saa 96.
Ripoti hiyo inasema, uamuzi huo unahusu picha kutoka nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, Iraq, Kuwait na maeneo jirani ya vita.
Kampuni hiyo imesema sababu ya uamuzi huo ni kuzuia uchambuzi kuhusu hasara zinazotokea katika kambi na vituo vya Marekani.
Kampuni ya Planet Labs yenye makao yake huko San Fransisco hutoa huduma ya picha za kiwango cha juu sana kwa serikali, makampuni na wachambuzi; na mara nyingi data zake hutumiwa kwa ajili ya kuchunguza hasara za mashambulizi ya kijeshi au mabadiliko ya nyanjani.
Katika miaka ya karibuni picha za satalaiti za kibiashara zimekuwa mojawapo ya vyanzo vikuu vya uchambuzi wa vita, na watafiti na vyombo vya habari vinatumia picha hizo kuchunguza na kutathmini hasara za kambi za kijeshi, viwanja vya ndege na taasisi za kimkakati.
Ripoti zinaonyesha kuwa, mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani yamesababisha hasara kubwa na hali na mali.
Novemba mwaka 2023 ripoti zilionyesha kwamba makampuni ya huduma za picha za satalaiti za kibiashara kama Planet Labs zilificha na kuchelewesha picha halisi za vita vya Israel, Ukanda wa Gaza.