Washington Post: Trump anakabiliwa na "upande mweusi" wa vita na Iran; majeneza yameanza kuwasili
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137238-washington_post_trump_anakabiliwa_na_upande_mweusi_wa_vita_na_iran_majeneza_yameanza_kuwasili
Gazeti la Washington Post limeitaja shughuli ya kupokea miili ya wanajeshi sita wa Marekani waliouawa katika operesheni kali ya Iran kuwa ni ishara kwamba vita vinamwendea vibaya rais wa nchi hiyo.
(last modified 2026-03-08T09:24:20+00:00 )
Mar 08, 2026 09:24 UTC
  • Majeneza ya wanajeshi wa Marekani waliouawa na Iran
    Majeneza ya wanajeshi wa Marekani waliouawa na Iran

Gazeti la Washington Post limeitaja shughuli ya kupokea miili ya wanajeshi sita wa Marekani waliouawa katika operesheni kali ya Iran kuwa ni ishara kwamba vita vinamwendea vibaya rais wa nchi hiyo.

Katika shughuli hiyo iliyofanyika jana Jumamosi katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Dover huko Delaware, Rais wa Marekani, Donald Trump alikutana na familia za wanajeshi sita wa akiba wa Jeshi la Marekani waliouawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Iran kwenye kambi yao huko Kuwait.

Gazeti la Marekani "The Washington Post" limetaja shughuli hiyo ya kupokea miili ya wanajeshi sita wa Marekani waliouawa katika operesheni kali ya Iran kuwa ni ishara kwamba vita vinamwendea vibaya Donald Trump, na limetoa tahadhari kuhusu mwenendo unaoendelea wa wanajeshi wa Marekani kuuawa, na Washington kujikuta katika dimbwi jingine la vita huko Asia Magharibi.

Gazeti la Washington Post limeandika katika makala yenye kichwa cha habari: Kurudi kwa Miili ya Wamarekani Waliouawa kwenye Vita vya Iran ni Ishara ya Trump Kukabiliana na Upande Mbaya wa Vita: “Huu ni ukurasa wa kwanza wa vita vinavyozidi kuongezeka ambavyo vinapindua meza kwa watu wa Marekani na urais wa Trump. Bado haijabainika matokeo ya vita hivi yatakuwaje.”

Gazeti hilo limeongeza: "Misimamo kutangatanga ya Trump kuhusu mwenendo wa operesheni dhidi ya Iran inaonyesha kwamba yeye mwenyewe hana uhakika wa matokeo ya vita hivi."

Akiwa amesimama karibu na ndege ya usafirishaji ya kijeshi, Trump alitoa heshima kwa majeneza yaliyofunikwa bendera za Marekani ya wanajeshi sita waliouawa na Iran na kusema: "Nachukia kufanya hivi, lakini ni sehemu ya vita."

Hata hivyo waangalizi wengi wanasema tukio hilo lilikuwa ukumbusho wa "upande mweusi wa vita" vya kiongozi huyo dhidi ya Iran.

Marekani na vyombo vya habari vya nchi hiyo vinajizuia kutangaza idadi halisi ya wanajeshi waliouawa katika mashambulizi ya Iran, lakini baadhi ya duru huru zinasema hadi sasa mamia ya wanajeshi wa Marekani wameuawa katika vita hivyo.

Sasa, wachambuzi wengi na Wabunge wa Marekani wanaonya kwamba ikiwa mkondo wa sasa utaendelea, huu unaweza kuwa mwanzo wa kurudi kwa majeneza mengi ya wanajeshi wa Marekani.