Russia yawasilisha rasimu ya azimio Baraza la Usalama, yataka kukomeshwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran
-
Baraza la Usalama
Russia imewasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikitaka kukomeshwa vita katika eneo la Asia Magharibi.
Vyanzo vya kidiplomasia vimetangaza kuwa, Russia imewasilisha rasimu ya azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikizitaka pande zote kusitisha mzozo huo na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Rasimu iliyopendekezwa na Russia inasema kwamba Baraza la Usalama "linahimiza vikali pande zote husika kurudi kwenye mazungumzo bila kuchelewa na kutumia kikamilifu nyenzo za kisiasa na kidiplomasia."
Rasimu hiyo imeongeza kuwa: Baraza la Usalama, linasisitiza tena madhumuni na kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa, likikumbuka kifungu cha 2(4) cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kinakataza matumizi ya nguvu dhidi ya ardhi au uhuru wa kisiasa wa nchi yoyote.
Rasimu hiyo iliyotayarishwa Russia inasisitiza kwamba: Baraza la Usalama "linalaani kwa lugha kali mashambulizi yote dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, linatoa wito wa kulindwa kwao, na linasisitiza tena wajibu wa pande zote wa kuheshimu sheria ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria ya kimataifa ya kibinadamu."
Sehemu nyingine ya rasimu ya azimio la Baraza la Usalama iliyopendekezwa na Russia inasema kwamba Baraza la Usalama "linasisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa nchi zote katika eneo la Asia Magharibi na zaidi ya eneo hilo."
Mashambulizi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo yamepelekea kuuawa shahidi Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yalianza asubuhi ya Februari 28, 2026. Uchokozi huo ulifanyika wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yakiendelea kwa upatanishi wa baadhi ya nchi za kikanda.