Russia: Iran ina haki ya kujitetea mbele ya mashambulizi ya Marekani, Israel
-
Maria Zakharova
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kujitetea na kukabiliana na hujuma za Marekani na Israel na ametoa wito wa kusitishwa mashambulizi ya Marekani na Israel na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Maria Zakharova amesema, kwa mujibu wa Mada ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, Iran kama zilivyo nchi nyingine, inayo haki ya kujitetea mbele ya hujuma za kijeshi za Marekani na Israel. Amesema: Moscow inaitaka Marekani na Israel kukomesha mashambulizi na kurudi kwenye meza ya mazungumzo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema, Moscow itaendeleza hatua zake kwa ajili ya kusitishwa mapigano haraka katika eneo la Magharibi mwa Asia na kutafuta suluhisho la hitilafu zilizopo kwa kutumia njia za amani.
Kuhusu mapendekezo ya Russia kwa ajili ya kusitishwa mashambulizi dhidi ya Iran na kukomeshwa mgogoro wa Asia Magharibi, Maria Zakharova amesema: “Tumetayarisha mapendekezo yanayofaa na kwa sasa tunafanya mawasiliano kuhusiana na kadhia hii.”