Dkt Tedros: Kushambulia kwa mabomu hospitali na shule ni jinai ya kivita
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137386-dkt_tedros_kushambulia_kwa_mabomu_hospitali_na_shule_ni_jinai_ya_kivita
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Duniani (WHO) amelaani vikali kitendo cha kushambuliwa kwa mabomu hospitali na shule, akisisitiza kuwa hujuma hizo si kitu kingine ghairi ya jinai za kivita.
(last modified 2026-03-15T05:12:15+00:00 )
Mar 15, 2026 05:12 UTC
  • Dkt Tedros: Kushambulia kwa mabomu hospitali na shule ni jinai ya kivita

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Duniani (WHO) amelaani vikali kitendo cha kushambuliwa kwa mabomu hospitali na shule, akisisitiza kuwa hujuma hizo si kitu kingine ghairi ya jinai za kivita.

Dakta Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kueleza kuwa: Kupiga mabomu hospitali na skuli sio makosa ya kimahesabu. Kuua wahudumu wa afya si hasara inayohalalishika. 

Kadhalika Dakta Tedros ameeleza bayana kuwa, kuua raia kwa njaa si 'mkakati wa mazungumzo', lakini yote hayo ni jinai za kivita, na wala haziashirii kitu kingine chochote.

Haya yanajiri huku majeshi katili ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel yakiendelea kudondoshea mabomu shule, hospitali, na vituo vya afya yakiwemo majengo ya Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Iran katika vita vyao vya kichokozi zilivyovianzisha Februari 28. 

Kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani, mashambulizi ya kinyama ya Marekani na utawala wa Kizayuni ambayo yameingia wiki ya tatu sasa, mpaka sasa yamelenga makazi na miundomsingi ya kiraia zaidi ya 43,000.

Mohajerani amesema hujuma hizo za kichokozi za Marekani na Israel zimelenga majengo 36,489 ya makazi ya watu, yakiwemo 10,000 jijini Tehran, vituo vya afya na dharura 43, ambulensi 32, na shule zaidi ya 120, ikiwemo Shule Msingi ya Minab huko kusini mwa Iran, ambapo wanafunzi wadogo wa kike zaidi ya 160 waliuawa shahidi.

Maseneta Elizabeth Warren na Chriss Van Hollen wa Marekani wametoa wito wa kutimuliwa Waziri wa Vita wa nchi hiyo, Pete Hegseth, kwa kutenda jinai hiyo ya kuua watoto wadogo wa Shule ya Msingi ya Minab, baada ya uchunguzi wa awali wa Pentagon kuonyesha kuwa Washington ndiyo iliyofanya shambulizi hilo lililolenga shule hiyo ya wasichana hapa nchini.