"Israel inadanganya, Iran haitutishii": Afisa wa ujasusi aliyeteuliwa na Trump ajiuzulu kwa sababu ya vita na Iran
-
Joseph Kent
Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi nchini Marekani amejiuzulu baada ya kufichua yanayojiri nyuma ya pazia kuhusu vita vya nchi hiyo na Israel dhidi ya Iran.
Joseph Kent alitangaza jana Jumanne kwenye mtandao wa kijamii "X" kwamba anajiuzulu kutoka kwenye wadhifa wake baada ya kufichua yaliyojiri nyuma ya pazia kuhusu mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Kent amefichua kwamba: "Iran si tishio la moja kwa moja kwa Marekani na ni wazi kwamba tumeanzisha vita hivi kutokana na mashinikizo ya Israel, kwa hivyo ninajiuzulu wadhifa wangu." Ameongeza kwa kusema: "Nimeamua kujiuzulu kwa sababu siwezi kuunga mkono vita vinavyoendelea dhidi ya Iran."
Katika barua yake kali kwa Rais Donald Trump, Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi cha Marekani amesema: Maafisa wakuu wa Israel na watu kadhaa wenye ushawishi katika vyombo vya habari vya Marekani walianzisha kampeni iliyopangwa ili kupotosha umma. Kampeni hiyo ilitumika kukudanganya uamini kwamba Iran ni tishio la moja kwa moja kwa Marekani.
Kent ameongeza katika barua yake kwa Trump: "Maneno ya kupata ushindi mwepesi na wa haraka iwapo tutashambulia Iran yalikuwa uongo mtupu. Hii ndio mbinu ile ile iliyotumiwa na Waisraeli hapo awali kutuingiza katika Vita vya Iraq vilivyokuwa na maafa vilivyoligharimu taifa uhai wa maelfu ya wanaume na wanawake bora. Hatuwezi kufanya kosa hilo tena"
Afisa huyo wa ngazi za juu wa serikali ya Trump amesisitiza: Siwezi kamwe kuunga mkono kupeleka kizazi kijacho cha vijana wa nchi yetu kwenye vita ambavyo havitakuwa na faida yoyote kwa watu wetu wala havihalalishi hasara za roho za Wamarekani.
Joseph Kent, anayetajwa kuwa mwanasiasa wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali, alithibitishwa katika wadhifa wa Mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi Marekani Julai mwaka jana kwa wingi wa kura 52 dhidi ya 44 za baraza la Seneti.
Akiwa mkuu wa Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi, Kent alikuwa na jukumu la kuchambua na kugundua vitisho vya kigaidi.
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Marekani, Joseph Kent ana uzoefu mkubwa katika masuala ya kupambana na ugaidi na utumishi wa kijeshi, akiwa ameshiriki katika vita mara 11 wakati wa kazi yake ya miaka 20 jeshini kabla ya kustaafu na kuwa afisa katika Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA).