Sauti na nara za kupinga vita dhidi ya Iran zasikika kuanzia Uhispania hadi Canada
-
Maandamano ya Wahispania dhidi ya vita vya Marekani
Wananchi wa Uhispania wameandamana kulaani vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran. Maelfu ya wananchi wa Uhispania wamemiminika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Madrid, kutangaza upinzani wao kwa vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Waandamanaji huko Madrid walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na maandishi ya kupinga vita dhidi ya Iran. Aidha wamepiga nara kupinga sera za Rais Donald Trump wa Marekani na mafashisti duniani.
Irene Montru mwakilishi katika Bunge la Ulaya kutoka chama cha siasa nchini Uhispania ambaye alishiriki katika maandamano hayo mjini Madrid ameitaka serikali ya Uhispania kuiondoa nchi hiyo katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) na kuondoka wanajeshi wa Marekani katika kambi za kijeshi za Rota na Moren dela Frontra huko Uhispania.
Ametahadharisha kuwa Hispania inashiriki katika vita vya sasa madhali ipo ndani ya muungano wa Nato; tutake tusitake sisi ni washirika katika jinai za Trump na Netanyahu madhali wanajeshi wa Marekani bado wapo katika kambi za Uhispania.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Elimu Jamii cha Uhispania (CIS); asilimia 69 ya wananchi wa Uhispania wanapinga vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran.