Uungaji mkono wa Wamarekani kwa utendaji wa Trump wapungua hadi asilimia 33
Uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani unaonyesha kuwa, kiwango cha uungaji mkono wa wananchi kwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwa mara nyingine tena kimepungua hadi asilimia 33 tu; huku idadi kubwa ya Wamarekani wakipinga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Tovuti ya Hill imeandika kuwa, uungaji mkono wa wananchi kwa utendaji wa Trump umepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani, huku idadi ndogo ya washiriki katika uchunguzi huu wa maoni wakisema wanaunga mkono hatua za kivita dhidi ya Iran.
Uchunguzi huo mpya wa maoni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Amhherst cha Massachusetts na matokeao yake kutangazwa siku ya Jumatatu unaonyesha kuwa asilimia 62 ya wapiga kura wa Marekani hawakubaliani na utendaji wa Trump, na asilimia 53 kati ya hao wanapinga vikali utendaji wa kiongozi huyo.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa asilimia 33 ya waliohojiwa katika uchunguzi huo mpya wa maoni nchini Marekani wameeleza kuwa "kwa kiasi fulani" au "sana" wanakubaliana na kauli mbiu ya kampeni ya Trump ya "Making America Great Again." Waungaji mkono wa nara hiyo ni pamoja na asilimia 77 ya Warepublican ambao ni wanachama wa chama cha Trump, ikilinganishwa na asilimia 4 tu ya Wademocrat.