Seneta wa Marekani: Mr. Trump, Mlango Bahari wa Hormuz haufunguliwi kwa matusi
-
Seneta "Ed Markey" wa Massachusetts
Seneta wa Marekani amekemea vitisho na matusi ya Rais wa nchi hiyo, Donald Trump dhidi ya Iran, akisema: Mlango Bahari wa Hormuz haufunguliwi kwa matusi na lugha chafu, bali ni lazima kufanya mazungumzo na Iran.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Seneta "Ed Markey" wa Massachusetts, Jumapili usiku, akijibu vitisho na matusi ya Trump kwenye akaunti yake ya X, ameandika: Tweet iliyojaa lugha chafu ambayo inatishia kufanya uhalifu wa kivita, haitafungua Lango Bahari la Hormuz. Kitu pekee kitakachofanya hivyo ni mazungumzo na Iran.
Seneta huyo wa Marekani amemuonya Trump akisema: "Donald, anza kwa njia ile ile ambayo mwishowe utalazimika kuifuata ili Wamarekani wasilazimike kununua petroli kwa bei ghali zaidi na majeshi yetu yasipoteze maisha.
Kabla ya hapo, jarida la kila wiki la The Week liliandika katika ripoti kwamba: Lango Bahari la Hormuz limeendelea kufungwa, na suala hili linasababisha shinikizo kubwa kwa masoko ya kimataifa ya nishati. Sehemu moja ya ripoti ya jarida hilo la Uingereza, ambalo pia linachapishwa kwa wakati mmoja huko nchini Marekani, imesema: Kadiri vita vilivyoanzishwa na Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya Iran vinavyoendelea, inazidi kubainika kwamba hakuna mkakati mkuu wa wazi katika mzozo huu, na sasa umegeuka kuwa vita vya kumomonyoana.
Wachambuzi wanaamini kuwa Ikulu ya Rais wa Marekani, White House sasa, badala ya kuzingatia lengo la mwisho lililo wazi, inajaribu kutengeneza njia mpya ya mashinikizo dhidi ya Tehran kwa hatua za muda mfupi.
Kwa sasa, Marekani inaendelea na mashambulizi yake dhidi ya shabaha na miundombinu ya kiraia ndani ya Iran, na wakati huo huo inatuma wanajeshi zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Kwa upande mwingine, Iran pia imeendelea kujibu mapigo kwa kushambulia maeneo mbalimbali ya Israel na maslahi ya Marekani katika baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi.