Shambulio la Utawala wa Kizayuni Dhidi ya Msafara wa Meli wa Sumud; Mijibizo, Jumbe na Matokeo Yake
Wanajeshi wa Kizayuni kwa mara nyingine tena wameushambulia msafara wa Sumud wa meli za kimataifa na kuzuia kupelekwa misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Ghaza uliowekewa mzingiro na utawala wa kizayuni wa Israel.
Wahusika wa msafara huo wa vyombo vya majini wa Sumud wametangaza kuwa, Wazayuni wameziharibu na kuzitelekeza meli 21 za msafara huo wa meli za kiraia. Wamewaacha baadhi ya wanaharakati wa kiraia waliokuwemo kwenye meli hizo wakiwa wamekwama na kutangatanga majini na kuwateka nyara wengine kadhaa.
Suali linaloulizwa hapa ni: walimwengu wametoa mijibizo gani kwa shambulio lililofanywa na wazayuni dhidi ya msafara wa Sumud wa meli za kimataifa, na tukio hilo linafikisha ujumbe gani na litakuwa na matokeo yapi?
Mbali na makundi ya Muqawama ya Palestina, Hizbullah ya Lebanon pia imelaani shambulio la kivamizi lililofanywa na wanajeshi wa utawala wa kizayuni dhidi ya msafara wa meli wa Sumud uliokuwa na lengo la kupeleka misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa Ghaza wanaoteseka na kuvunja mzingiro waliowekewa wananchi hao madhulumu na utawala huo dhalimu. Hizbullah ya Lebanon imetangaza katika taarifa kwamba, kitendo cha utawala wa Kizayuni cha kuzishambulia meli za msafara wa kimataifa wa Sumud na kuzikamata meli hizo katika maji ya kimataifa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kinahesabiwa kuwa ni uharamia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki nayo pia imetangaza kwamba uingiliaji uliofanywa na Israel dhidi ya msafara wa meli za misaada zilizokuwa zikielekea Ghaza ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na maadili ya kibinadamu. Aidha, Ankara imebainisha kuwa hatua hiyo inakiuka kanuni ya uhuru vilionao vyombo vya baharini wa kufanya safari katika maji ya kimataifa.
Francesca Albanese, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Haki za Kibinadamu katika Palestina, yeye pia amelaani hujuma iliyofanywa na utawala wa kizayuni katika maji ya kimataifa dhidi ya msafara wa kimataifa wa vyombo vya baharini wa Sumud na kubainisha: "msafara wa meli wa Sumud umeshambuliwa katika maji ya kimataifa. Utawala wa kizayuni ni wa ubaguzi wa rangi, na viongozi wa utawala huo wamefanya jinai ya mauaji ya kimbari."
Shambulio dhidi ya msafara wa Sumud lina nukta na jumbe muhimu pia linazofikisha. Moja ya jumbe hizo ni kwamba, kutokana na kuungwa mkono na Marekani na kwa sababu ya udhaifu lilionao Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kutoweza kuchukua hatua yoyote, utawala wa kizayuni haujali wala hauhofu chochote kuhusiana na kuendeleza jinai za kivita dhidi ya watu wa Ghaza.
Ujumbe mwingine muhimu ni kuwa, kinyume na inavyodai serikali ya Marekani kwamba imeweza kuhitimisha vita dhidi ya Ghaza, ukweli ni kuwa, vita hivyo bado havijamalizika na vingali vinaendelea kwa sura ya mzingiro wa pande zote lililowekewa eneo hilo la Wapalestina na utawala wa kizayuni.
Shambulio dhidi ya msafara wa kimataifa wa meli za misaada ya kibinadamu wa Sumud lina athari na matokeo muhimu pia. Miongoni mwa matokeo muhimu zaidi ya hujuma hiyo ni kuthibitika udhaifu wa jamii ya kimataifa na hasahasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kutoweza kusimamisha jinai za kivita zilizoenea, zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ghaza. Kwa hakika, hatua ya Wazayuni dhidi ya msafara wa meli wa Sumud ni mwendelezo wa hatua zinazoudharaulisha na kuutoa thamani Umoja wa Mataifa duniani.
Matokeo mengine muhimu ya shambulio hilo ni kuonyesha kwamba, kutokana na jinai za utawala wa Kizayuni, likiwemo shambulio dhidi ya meli za msafara wa Sumud zilizokuwa zimebeba raia 400 zikiwa na lengo la kupeleka misaada ya kibinadamu huko Ghaza, maadili ya binadamu na tunu za haki za binadamu zinaendelea kukabiliwa na mwenendo wa uharibifu na uporomokaji.
Nukta ya kumalizia ni kwamba, hii si mara ya kwanza na wala haitakuwa ya mwisho kwa msafara wa kimataifa wa meli za Sumud kushambuliwa na utawala wa Kizayuni. Shambulio hilo litarudiwa tena katika siku za usoni, kama ilivyotokea huko nyuma kwa misafara mingine ya meli za misaada ya kibinadamu iliyokusudiwa kupelekwa huko Ghaza kupunguza machungu na mateso ya Wapalestina.
Na matokeo ya mashambulizi hayo yatakuwa ni kuendelea kuongezeka ghadhabu na chuki za walimwengu kwa utawala wa Kizayuni, na wakati huo huo kupanua ufa wa mpasuko uliopo kati ya fikra za umma kimataifa na madola makubwa kutokana na madola hayo kutokuwa na nia ya kukomesha jinai za utawala huo ghasibu.../